BORA ZIWE ZA UKWELI
1. Dunia geuka nyuma, angalia Tanzania,
Tunaleta usalama, huko mlikofulia,
Ipokee dawa njema, korona itaishia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
2. Kufa kufaana jama, dawa yetu yaingia,
Kuokoa kina mama, na akina baba pia,
Hatutajali gharama, afya itaifidia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
3. Mbona tutacheza ngoma, korona ikififia,
Tufanye mambo ya chama, tuchague wenye nia,
Sasa yatutia homa, kampeni zinafifia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
4. Hamu haitaki hama, madawa kujipatia,
Ugonjwa uweze koma, kwetu kutufwatilia,
Watoto waende soma, muda wao kufidia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
5. Hivi tulivyochutama, dawa tukisubiria,
Bora tusishike tama, muda ukatuishia,
Kama dingi avosema, kazi tufanye kwa nia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli,
6. Kwa sasa dunia nzima, gonjwa limetufikia,
Kote kote twachagama, maisha twapigania,
Japo dawa imegoma, njia nyingi twatumia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
7. Maagizo tumesoma, kazi tunayafanyia,
Virusi vipate koma, kule kutushambulia,
Yasitufike ya Roma, tukazidisha kulia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
8. Watalamu nchi nzima, bora maji kuvulia,
Ogeni mwili mzima, dawa kututafutia,
Pengine yetu salama, iko hapa Tanzania,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
9. Kokote dunia nzima, wale wenye njema nia,
Watafute usalama, kukiwepo kuchanjia,
Ili tusije kuzama, kwa vifo kutuzidia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
10. Mungu tunakutazama, wewe ndiye mwenye njia,
Tumepigwa tumekoma, sasa kama twatitia,
Neno moja wewe sema, ahueni tatujia,
Habari za dawa hii, bora ziwe za ukweli.
Na Lwaga Mwambande
© Kila Mwenye Pumzi Amsifu Bwana (KiMPAB) 2020
0767223602