Watoto wa familia moja mtaa wa Rungwa Manispaa ya Mpanda wakiwa wamekaa juu ya tofali zilizobomoka kutoka katika nyumba yao baada ya mvua kunyesha
Mabaki ya iliyokuwa nyumba ya familia ya kina Agnes
………………………………………………………………………..
Na. Zillipa Joseph,Katavi
Kaya nne za mtaa wa Rungwa kata ya Kawajense katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi zimeiomba serikali kuwasaidia fedha na mabati kwa ajili ya kujenga nyumba zao zilizobomolewa na mvua wiki moja iliyopita
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wahanga hao wamesema kwa sasa wanaishi kwa jamaa zao wakati wakijipanga kuanza ujenzi upya
Agnes Pambe ni mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Rungwa; anatoka katika moja ya kaya zilizoathirika, anasema alikuwa na wadogo zake watatu wakati mvua inanyesha kisha ukuta wa chumba ukaanguka
“Tulikimbilia nje mvua ikiendelea kunyesha na daadae nyumba yote ilianguka” alisema Agnes
Amesema anaishi na wadogo zake wanne; wawili kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka saba na kuongeza kuwa mama yao anafanya kazi ya kupika mgahawa katika kata ya machimboni na hivyo huja kuwasalimu kila akipata nafasi
Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Rungwa bi. Felicia Mkota amesema alilazimika kuwatafutia watoto mahali pa kuishi kwa msamaria mwema, mpaka mama yao alipokuja baada ya siku tano na kuwapangishia chumba