……………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota(CCM) ameiomba Wizara ya Nishati kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi majumbani ili kuwanufaisha wananchi na kuwapunguza gharama za maisha.
Chikota ametoa ombi hilo leo bungeni alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2020/21.
Amefafanua kuwa miradi mingine ya umeme imesimamiwa kikamilifu lakini usambazaji gesi majumbani bado kasi yake hairidhishi.
“hadi sasa gesi imefika kwa vijiji 425 lakini kuna mitaa mingine ya na Mangowela ambavyo vipo maeneo yaliyotakiwa kufikiwa lakini akashangaa mitaa hivyo kutofikiwa,”amesema.
Ameeleza kuwa pamoja na uzuri wa Wizara hiyo usambazaji wa gesi majumbani mchakato wake bado haukidhi mahitaji licha ya kuwa wamepeleka vijiji vingi hivyo kasi iongezwe.
Mbunge huyo amefafanua kuwa hadi sasa malalamiko katika jimbo lake yamepungua na kwamba usambazaji wa umeme umeleta matumaini kwa wananchi kutokana na kufika katika maeneo mengi kwa wakati huu.
Aidha, amemuomba Waziri kutosikiliza kauli za baadhi ya wanasiasa na wabunge kuhusu meneja wa umeme wa mkoa wa Mtwara kwamba hafanyi kazi si za kweli na kueleza kuwa ni mtu anayechapa kasi usiku na mchana na anastahili kupandishwa cheo.
Kwa upande wake,Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia(CCM) amesisitiza kuwa kasi ya usambazaji umeme vijijini ni kubwa na kwamba kasi hiyo itatoa kura kwa asilimia 88 kwenye uchaguzi huu ujao kwa viongozi wa serikali kutoka kwa wananchi wa eneo hilo.