Watoto Abigaeli na Roselyn wakiwasha moto kwa kutumia magunzi ya mahindi ili wapike chakula chao. Hawa ni wakazi wa Makanyagio na wazazi wao wameenda kuvuna mpunga
***********************************
Na Zillipa Joseph, Katavi
Wazazi wa mkoa wa katavi wametakiwa kutowaacha watoto wajilee peke yao hasa katika msimu huu wa kilimo wakati wao wakiwa mashambani wanalima
Hali hii imeelezwa kusababisha matatizo kadhaa kama watoto kujiingiza katika tabia za wizi au kusababisha mimba za utotoni kutokana na watoto kuachwa peke yao au wakati mwingine wanaachwa na bibi yao ambaye anakuwa ni mzee sana
Bi. Magreth Mwaipasya ni mkazi wa mtaa wa Tulieni katika Manispaa ya Mpanda ameeleza kuwa aliwahi kukamata watoto wakiiba katika bustani yake
“Nilikamata watoto wawili wakichuma mboga katika bustani yangu, niliwafikisha hadi nyumbani kwao na kisha kwa mwenyekiti wa mtaa nikagundua walikuwa wanalelewa na dada yao anayesoma darasa la sita” alisema Magreth
Ameeleza kuwa watoto hao wa kiume (majina yanahifadhiwa) mmoja alikuwa na miaka saba na mdogo wake alikuwa na miaka mitano
Bwana James Msuya ameshauri wazazi kuwakumbuka watoto na kuwatembelea kila mara ili kuziba mapungufu yaliyo katika familia
“Unakuta toka novemba baba mama walihamia shamba wanategemea kurudi mwezi wa sita wakishavuna sasa hiyo ni mbaya hata kama unatuma hela jipe muda wa kuja kuwaona utaona mapungufu mengi tu” alisema Msuya
Baadhi ya watoto wameeleza kuwa wazazi wao wamesafiri kwenda kijijini kwa shughuli za kilimo na hivyo majirani wanawasaidia kuwaangalia
Nimebaki mimi na mdogo wangu ana miaka saba, kaka nae alienda shamba shule zilipofungwa, majirani wanatusaidia” alisema Abby mwenye umri wa miaka tisa
Akizungumzia suala hilo afisa maendeleo ya jamii mkoa wa katavi bi Anna Shumbi amekiri kuwepo kwa tabia hiyo kwa wakazi wa mkoa wa Katavi
Amesema wakazi wengi ni watu wenye kipato cha chini na wanategemea zaidi kilimo hali ambayo inawalazimu kuhamia mashambani msimu wa kilimo unapowadia
Ameongeza kuwa hali hiyo inachangia kuwa utoro wa shule, udokozi, uzururaji na hata wakati mwingine mimba za utotoni
“Unakuta mtoto aliyeachwa kulea wenzie ni wa kike, fedha zinapoisha ni rahisi kurubuniwa na mwenye duka na akashiriki nae ngono ili wapate chakula” alisema
Aidha amewashauri wazazi kujenga tabia ya kuwaacha watoto na mtu mzima mwenye akili timamu na nguvu za kuwasimamia watoto ili kuwalinda na athari ambazo zinaweza kujitokeza