Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi.Zainab Telack akikagua vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Corona vilivyotolewa na Shirika la World Vision huku Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Ziwa Bw. John Massenza akiangalia.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndugile akiongea na vyombo vya habari wakati wa kukabidhiwa vifaa vya kujikinga na corona mapema leo mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi.Zainab Telack katikati akikagua vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Corona vilivyotolewa na Shirika la World Vision leo mkoani Shinyanga kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Yudas Ndungile na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Ziwa Bw. John Massenza.
Mkurugenzi wa Shirika la World Vision Kanda ya Ziwa Bw. John Massenza akiongea na vyombo vya habari wakati wa kukabidhi vifaa vya kujikinga na corona mapema leo mkoani Shinyanga.
*******************************
NA Mwandishi wetu Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amepokea msaada wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Corona wenye thamani ya Shilingi Milioni 29 kutoka shirika la World Vision Kanda ya Ziwa kwa ajili ya watumishi wa Afya walioko mstari wa mbele kupambana na ugonjwa huo katika mkoa wa Shinyanga.
Akiongea mara baada ya makabidhiano ya vifaa hivyo Bi. Zainab Telack amesema kuwa vifaa hivyo ni msaada mkubwa kwa waudumu wa afya kwani vitawasaidia wafanyakazi hao kuwaudumia wagonjwa wa corona kwa amani kwa kuwa watakuwa na uhakika wamejikinga ipasavyo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa baadhi ya vifaa vilivyotolewa na Shirika hilo vitawezesha pia watendaji kutoa elimu kwa wananchi wakiwa mbali bila kulazimika kuwa katika msongamano kwani shirika hilo limechangia pia vipaza sauti kwa ajili ya kutoa elimu maeneo ya vijijini.
Bi. Zainab Telack amewataka waudumu wa afya pamoja na wananchi kwa ujumla wasichoke na kuendelea kujikinga na kuwakinga wengine kwa kuwa ugonjwa wa corona hauchagui lakini pia haujulikani uko kwa nani nakuwataka wadau, wananchi pamoja na serikali kushiriki katika mapambano dhidi ya corona.
Akiongea na waudumu wa Afya mara baada ya kukamilisha kazi ya kupokea vifaa hivyo Bi. Zainabu Telack aliwataka waudumu hao kufikiria kutumia njia mbadala ikiwemo matumizi ya mitishamba iliyopendekezwa na wataalam wa Afya ikiwemo kujifukiza kwa kuwa ugonjwa huu mpaka sasa hauna tiba maalum iliyopendekezwa.
‘’Baadhi ya watu wametumia dawa za kujifukiza na kupata nafuu kubwa na ninyi tumieni dawa hizi kupambana na ugonjwa huu kwani kila mmoja wetu akifanya jitihada za kutokomeza ugonjwa huu tunaweza kuumaliza’.’ Alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkurugenzi wa Shirika la Word Vision Kanda ya Ziwa Bw. John Massenza amevitaja vifaa vilivyotolewa na shirika lake kuwa ni Gloves, Magauni ya Kujikinga, Vitakasa Mikono, Vipasa sauti pamoja na barakoa na kuongeza kuwa tayari Shirika lake limetoa mafunzo kwa watoa huduma ngazi ya jamii, vituo vya Afya na baadhi ya madiwani Wilayani Shinyanga.
Aidha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile ameshukuru uongozi wa Shirika hilo kanda ya Ziwa na kuwataka wadau wengine kuendelea kushirikiana na serikali kuchangia vifaa vya kujikinga na Corona na kuwezesha watoa huduma ya Afya kujikinga na kuwadumia wagonjwa kwa usalama na uhakika.
Serikali Mkoani Shinyanga inaendelea kuelimisha jamii ikiwemo kuhakikisha watu wanavaa barakoa pamoja na kuepuka misongamano katika minada ya mifugo ikiwemo kupiga maarufuku wazazi kwenda na watoto katika maeneo yenye mikusanyiko.