**********************************
Benki ya NMB kwa kushirikiana na Mastercard na kampuni ya utoaji huduma za usafiri – EYWA, wamezindua mfumo mpya wa malipo kwa njia ya kidijitali kwa wasafiri nchini Tanzania.
Mfumo huo unaojulikana kama ‘EYWA Transit Solution’, utawawezesha wasafiri kukata tiketi kwa njia ya kidijitali
kupitia simu za mkononi na kadi maalumu.
Suluhisho hili linalenga kutatua changamoto za huduma za usafirishaji nchini kwa kupunguza matumizi ya mfumo wa malipo ya fedha taslimu na kuwa katika njia ya kidijitali kwa mamilioni ya abiria wanaosafiri kila siku.
“Utaratibu huu wa malipo ni sehemu ya mikakati ya Benki ya NMB kurahisisha upatikanaji wa huduma
za kifedha kwa wadau wa sekta ya usafiri nchini,” alisema Ruth Zaipuna, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
benki ya NMB.
Kupitia huduma hii, wasafiri wataweza kuangalia muda wa safari, kupata taarifa fupi, kuscan kadi na
kuingia ndani ya basi bila kupanga foleni. Watumiaji wa smartphone wataweza kupakua program
maalumu kupata maelezo ya huduma hiyo jambo ambalo litazuia au kupunguza mawasiliano ya ana kwa
ana katika utoaji huduma za usafiri.
Watoa huduma za usafiri au wamiliki wa mabasi kwa upande mwingine wataweza kukagua orodha ya
abiria waliofika katika kila kituo, pia huduma hii itaokoa muda kwa sababu kabla ya abiria kuchukuliwa
kituoni ataweza kupewa taarifa idadi ya vituo vilivyosalia kabla ya basi kumfikia alipo.
Wasimamizi wa mabasi pia watafaidika kutokana na kujumuishwa katika mfumo wa kifedha wa kidijitali,
na kujipatia kumbukumbu za taarifa za kifedha ambazo mara nyingi huhitajika pindi wanapohitaji
mikopo kutoka taasisi za fedha.
Ili kufurahia huduma hii, abiria wote wataombwa kufuata kadi hizi maalumu za usafiririshaji – EYWA
watakazopatiwa bure kutoka kwa mawakala wa EYWA waliopo kwenye vituo vya mabasi. Huduma hii
itapatikana katika vituo vyote vya mabasi nchini ikianzia Dar es Salaam.
Kama mshirika wa huduma za kibenki katika ushirikiano huu, sio mara ya kwanza kwa Benki ya NMB
kuwezesha waendeshaji wa huduma za usafirishaji nchini kujiunga na uchumi rasmi unaotumia mfumo
wa malipo kwa njia ya kidijitali.
Mwaka jana Mastercard QR na NMB walizindua mfumo wa malipo unaowawezesha waendesha pikipiki kupokea malipo ya wateja wao moja kwa moja kutoka kwenye
akaunti zao za benki ya NMB.
Hii imewawezesha kuwa katika mfumo salama wa malipo ambao unawaingiza katika jukwaa moja la huduma za kifedha.