Home Mchanganyiko VYUO VYA KILIMO NCHINI VYATAKIWA KUJIIMARISHA KIMAPATO

VYUO VYA KILIMO NCHINI VYATAKIWA KUJIIMARISHA KIMAPATO

0

Katibu Mkuu Wizara ya Killimo Bw.Gerald Kusaya  (aliyevaa suti ya blu ) akiongea na Askari na Maafisa wa JKT Bulombora Kigoma alipotembelea kukagua utekelezaji wa agizo la Waziri  Mkuu kuhusu uzalishaji miche bora ya zao la mchikichi.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua shamba la mbegu bora ya mihogo inayozalishwa kwenye Kituo cha Wakala wa Mbegu (ASA) Bugaga wilayani Kasulu leo .

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa suti) akitizama shamba darasa la mapapai  katika chuo cha Kilimo Mubondo wilaya ya Kasulu alipotembelea chuo hicho leo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika chupa ya asali inayozalishwa na chuo cha Kilimo Mubondo wilaya ya Kasulu.Kushoto ni mkufunzi wa kilimo na ufugaji nyuki kibiashara Mwl.Elias Lubimbi akitoa maelezo .

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa anaongea na watumishi wa Chuo cha Kilimo ( MATI) Mubondo ( hawapo pichani) 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mche bora wa mchikichi aina ya Tenera unaozalishwa katika shamba la Wakala wa Mbegu (ASA) kituo cha Bugaga wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma hivi leo.

(Habari na Picha Wizara ya Kilimo)

************************************

Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo ( MATI) vimeagizwa kuhakikisha vinatumia wataalam wakufunzi na rasilimali ardhi kuzalisha mazao mengi bora ili kuwa na uhakika wa
kipato na kujiendesha kibiashara.

 

Agizo hilo limetolewa leo Jumanne na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya wakati alipotembelea Chuo cha Kilimo Mubondo Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma.

 

 “Tumieni sayansi kuzalisha mazao ya kilimo kwa kuhakikisha mnapima udongo na kujua virutubishi vinavyofaa ili mjue zao gani na aina gani ya mbolea ili kuwa na mavuno ya kutosha kuwezesha vyuo kujipatia mapato”. Kusaya.

 

Katibu Mkuu huyo alisema lengo la serikali kuanzisha vyuo vya mafunzo ya kilimo ni kufundisha vijana na wakulima wengi kanuni bora za kilimo ili waweze kutoa mchango katika kukuza sekta ya kilimo nchini.

 

Amevitaka vyuo hivyo kutumia vema ardhi iliyopo na teknolojia kutoa mafunzo bora na kuzalisha mazao kibiashara ili wanafunzi wanaohitimu waweze kuwa
mahili katika kujitegemea na kuongeza ajira kupitia kilimo na chuo kupata mapato
.
“Vijana wengi watakapofanya vema na kufanikiwa katika kuanzisha shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo ndio itakuwa nafasi ya vyuo hivi kujitangaza na kuvutia vijana wengine na wakulima kuja kujifunza”alisisitiza Katibu Mkuu huyo.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kilimo MATI Mubondo Hanif Nzury aliomba serikali ikipatie Chuo hicho trekta ili kiweze kutumia kuongeza uzalishaji zaidi wa
mahindi, alizeti na michikichi ombi ambalo Katibu Mkuu alilikubali na kuahidi kulifanyia kazi.

 

Aidha Katibu Mkuu Kilimo amewataka Maafisa Ugani kote nchini kuwasaidia wakulima kwa kuwatembelea na kuwapa ushauri juu ya kanuni bora za kilimo .

 

Katika hatua nyingine Kusaya ameziagiza taasisi zote chini ya Wizara ya Kilimo kuhakikisha wanashirikiana na Halmashauri nchini kupima maeneo hayo na kupata hatimiliki ikiwa na lengo la kuyaepusha na uvamizi toka kwa wananchi.

 

Wizara ya Kilimo inasimamia vyuo 14 vinavyotoa Mafunzo ya stashahada (Diploma) na astashahada ( Certificate) pamoja na vituo vya utafiti 17 nchini.

 

Awali Katibu Mkuu Kusaya alitembelea Shamba la mbegu bora la Bugaga lililopo Kasulu chini wa Walaka wa Mbegu (ASA) ambapo ameagiza wahakikishe miche 5000 ya michikichi iliyopo tayari hapa kituoni inawafikia wakulima kama alivyoagiza Waziri Mkuu.

 

“ Waziri Mkuu yuko mstari wa mbele kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mafuta ya kula hivyo endeleeni kuzalisha miche mingi ya michikichi ili wakulima wapande
na hatimaye tupate mavuno mengi yatakayotosheleza mahitaji ya mafuta” alisema Kusaya.