Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyeshika miche ) akikagua kitalu cha miche ya michikichi inayozalishwa na Gereza Kwitanga kwa ushirikiano na TARI Kihinga.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mche bora wa mchikichi uliozalishwa na Kituo cha utafiti TARI Kihinga mkoa wa Kigoma leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikagua kitalu cha miche bora ya zao la michikichi katika Gereza Kwitanga mkoa wa Kigoma leo alipotembelea kuona utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za michikichi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua vitalu vya miche bora ya zao la michikichi aina ya Tenera katika Gereza Kwitanga mkoa wa Kigoma leo.
(Picha na Habari na Wizara ya Kilimo)
***********************************
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo amewapongeza watafiti wa mbegu za michikichi kwa kuongeza uzalishaji
wa mbegu bora na kuwataka watumie muda mfupi zaidi wa kuzalisha na kuzisambaza kwa wakulima
nchini.
Agizo hilo limetolewa leo mjini Kigoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerald Kusaya wakati
alipotembelea kukagua kituo cha Utafiti wa kilimo ( TARI) Kihinga, Gereza Kwitanga na JKT Bulombola
zenye jukumu la kuzalisha miche bora ya michikichi aina ya Tenera.
“ Watafiti endeleeni na utafiti wa kupunguza muda wa kuzalisha mbegu bora toka miezi 18 hadi chini ya
mwaka mmoja ili wakulime wapate mbegu hizo kwa wingi waongeze uzalishaji kufikia lengo lililowekwa
la miche milioni tano kwa mwaka” alisema Kusaya
Kusaya alisema ametembelea mkoa wa Kigoma kufanya ufuatiliaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alilitoa mwezi Agosti mwaka 2018 la kuitaka wizara ya kilimo kuzalisha miche bora ya
michikichi milioni 20 kwa kipindi cha miaka minne na kugawa kwenye halmashauri za mkoa huo na
mikoa mingine ili nchi ipate mafuta ya kutosha ya kula.
Katibu Mkuu huyo alisema ni lengo la serikali kuona zao la michikichi linalimwa mikoa mingi zaidi na ili
kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini kwani zao hilo ndio tegemeo kubwa la viwanda vya
mafuta..
Awali Kusaya alisema kwa sasa Tanzania inatumia shilingi Bilioni 443 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula
nje ya nchi kutokana na uzalishaji wa mazao ya mafuta kuwa mdogo .
“ Kwa mwaka nchi inahitaji mafuta ya kula tani 570,000 wakati uzalishaji wa ndani ni tani 250,000 sawa
asilimia 36 hivyo kuwa na upungufu wa tani 220,000 “ alisema Katibu Mkuu huyo
Awali akiwasilisha taarifa ya Kituo cha TARI Kihinga Mkurugenzi Mkuu wa TARI Geofrey Mkamilo alisema
agizo la Waziri Mkuu limeanza kutekelezwa kwani kufikia Mwezi Aprili mwaka 2020 jumla ya mbegu
bora za michikichi 1,791,768 ambazo zinaweza kupandwa kwenye eneo la ekari 35,835.
Dkt.Mkamilo aliongeza kusema jumla ya mbegu za michikichi aina ya Tenera 1,255,111 na miche bora
167,315 imezalishwa na taasisi za umma na binafsi kutekeleza agizo la Waziri Mkuu.Mbegu hizo zina
uwezo wa kutoa mavuno tani 5 kwa hekta .
Nae Mkuu wa Gereza Kihinga SSP Dominic Kazmil alimweleza Katibu Mkuu kuwa jumla ya mbegu
273,050 zimezalishwa tayari na miche 8,050 ipo tayari kwenda kupandwa na wakulima kwenye
halmashauri za Mkoa wa Kigoma .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru
Wizara ya Kilimo kwa jitihada za kuhakikisha mkoa wa Kigoma unakuwa kitovu cha uzalishaji miche ya
zao la michikichi.
Katika ziara hii ya mkoa wa Kigoma Katibu Mkuu Kusaya ameuomba uongozi wa mkoa kuhamasisha
wakulima pamoja na kuzalisha michikichi sasa waanze pia kuzalisha mazao kama mkonge na korosho ili
kuongeza wigo wa mapato kwenye mazao ya biashara.
Kusaya alisema ni wakati sasa wataalam wa kilimo wakawaelimisha wakulima waongeze mazao mengine
ya biashara kama korosho na mkonge ili kuwa na uhakika wa kipato kwani ardhi ya Kigoma inafaa na
kuwa wizara yake ipo tayari kuleta mbegu bora za mkonge na korosho.