……………………………………………………………………
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI leo tarehe 04.05.2020 majira ya saa 05:00 Alfajiri amefanya ukaguzi wa kushtukiza wa Mabasi ya Abiria yanayofanya safari kwenda mikoa mbalimbali kabla ya kuanza safari kwa lengo la kuangalia usalama wa vyombo hivyo vya usafiri pamoja na kujiridhisha na usimamizi na utekelezaji wa maelekezo yake kwa wakaguzi wa magari waliopo Stendi Kuu.
Katika ukaguzi huo alikuta Mabasi matatu ya abiria yenye namba za usajili T.619 CQV aina ya Scania Mali ya Kampuni ya Isamilo Express linalofanya safari kati Mbeya – Mwanza ambalo tari zake zilikuwa zimeisha na lilikuwa na tatizo kwenye mfumo wa breki, Basi namba T.420 DNM aina ya Toyota Coaster Mali ya Kampuni ya Amazon Tour Express linalofanya safari kati ya Mbeya – Sumbawanga tairi zake zilikuwa zimeisha na Basi namba T.606 DLQ aina ya Euchre Mali ya Kampuni ya Gitu Express pia tairi zake zilikuwa zimeisha.
Kutokana na matatizo hayo, Kamanda MATEI alizuia mabasi hayo kuendelea na safari hadi yatakapofanyiwa marekebisho ikiwa ni pamoja na kuwekewa tairi mpya. Uongozi wa Kampuni ya Isamilo Express ulileta basi jingine la kampuni hiyo na abiria kuhamia kwenye basi hilo na kuanza safari, pia basi la kampuni ya Amazon Tour Express lilibadilishwa tairi na kuruhusiwa kuendelea na safari.
Aidha Kamanda MATEI amekagua usalama wa abiria kabla ya kuanza safari hasa kipindi hiki cha uwepo wa ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu [COVID 19] na kuwataka Madereva, Abiria na Uongozi wa Stendi Kuu ya Mabasi Mbeya kuhakikisha kila mmoja anafuata maelekezo yanayotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi pamoja na Wizara ya Afya hususani kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka yenye sabuni au vitakasa mikono [Sanitizer] ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu.
Aidha Kamanda MATEI ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanafanya matengenezo mara kwa mara ya vyombo hivyo kabla na baada ya safari ili kujiridhisha juu ya usalama wake. Pia amewataka abiria kutoa taarifa za mienendo ya mabasi hayo kwa Jeshi la Polisi kupitia namba za simu ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya madereva wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.