Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh. Kalolo Ntila
Baadhi yaWataalamu waliohudhuria kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini.
********************************
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh. Kalolo Ntila amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo juu ya kusuasua kwake kuwachukulia hatua watumishi ikiwemo watendaji wa vijiji wanaokwamisha utekelezaji wa maazimio na mipango mbalimbali ya halmashauri hali inayopelekea kukwamisha maendeleo ya wananchi.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa baraza hilo limekuwa likimuagiza Mkurugenzi ambaye ndiye katinbu wa vikao vya baraza kutekeleza maazimio kadhaa ikiwemo kuwawajibisha watumishi wasio waadilifu hasa katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri lakini mrejesho wa maazimio hayo umekuwa sio wa kuridhisha, jambo ambalo madiwani hao hawaridhiki nalo.
“Na sisi tunampenda sana ndugu yetu Mkurugenzi, lakini kama anaweza kawaacha wadogo zake wakamfikisha pahali pa hovyo, pia anahatarisha kibarua chake, kumbe wakati mwingine ukimuona mdogo anafanya vya hovyo ni vizuri kuchukua hatua ili ugali wako pia uendelee kuwepo, kwasababu mwisho wa siku sisi hatuji kumtafuta mtumishi mmoja mmoja, Tunaempa maelekezo haya ni Mkurugenzi Mtendaji, na yeye anajua akina nani wanafanya hivyo,lakini kama anaweza akatuletea kwamba hawa sisi wanatukwamisha, sisi tuna meno, hawa ni maji maramoja tu ” Alisisitiza.
Awali wakati akichangia hoja hiyo Diwani wa kata ya Kaengesa Mh. Godfrey Kauzeni alisema kuwa kwa muda mrefu baraza hilo limekuwa likitoa maazimio lakini hakuna utekelezaji hali inayopelekea kila siku kutoa maazimio hayo kwa hayo ilihali madiwani wenyewe ndio wasimamizi na kuongeza kuwa huenda wao kama wasimamizi wanachelewa kuchukua hatua.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa umakini wako wewe mwenyewe, kama tukisimama vizuri katika kusimamia hizi hoja, zikajibiwa kwa wakati na pale ambapo kunaonekana kuna kuchelewa, wapo wanaochelewesha, kwanini tunawaacha tusichukue hatua, pengine na sisi chombo hiki tumekuwa wapole sana, pengine Mkurugenzi alishajua namna tulivyo, kwahiyo naacha tu bora liende tu, kwasababu anajua hakuna ‘action’ zozote zitakazochukuliwa,” Alisema.
Hayo yamesemwa katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini.
Akizungumza kabla ya kufungwa kwa baraza hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amelisisitiza baraza hilo kuwa na uwezo wa “kung’ata” pale inapobidi baada ya kuona utekelezaji wa maazimio hayajatekelezwa kama mlivyokubaliana na kuongeza kuwa kuazimia ni jambo moja lakini ufuatiliajia wa maazimio hayo ni jambo jingine ambalo linapaswa kufanyika.
“Kwahiyo nikazie tu kwamba, lazima baraza ling’ate, baraza lisimamie maazimio yake kuhakikisha kwamba yametekelezwa tena kikamilifu, kwasababu mlipokaa na kutoa maazimio mlikuwa mko ‘serious’ sasa hiyo ‘seriousness’ lazima iwepo pia kwenye kutekeleza yale maazimio ambayo sasa ni kazi ya Mkurugenzi, sasa ni lazima muudhibiti upande huu wa Menejimenti, ni jukumu la kwenu hilo la kiusimamizi,” Alieleza.
Kwa mujibu wa taarifa za mfumo wa ukusanyaji wa mapato, hadi tarehe 23 Aprili, 2020 makusanyo yatokanayo na mashine za Point Of Sales (POS) ambayo hayajapelekwa benki ni shilingi 509,033,302/= huku waheshuimiwa madiwani wakiidai halmashauri hiyo shilingi 175,000,000/= ambayo wanatakiwa kulipwa kabla ya tarehe 30.5.2020.