***********************************
Na Ahmed Mahmoud, Arusha
Imeelezwa kuwa changamoto ya utoaji wa fedha za fidia kwa nchi zenye kuleta athari ya mabadiliko ya Tabianchi duniani kwa kiwango kikubwa imekuwa ni Tatizo hivyo inahitajika mjadala mpana kuokoa hali ya athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa nchi changa duniani.
Hayo yamebainishwa kwenye mjadala wa kamati ya Kilimo Maliasili na Utalii ya bunge la Afrika mashariki na mbunge wa bunge hilo Josephine Lemoyan wakati alipokuwa akiongea na vyombo vya habari Mara baada ya kikao Chao kwa njia ya Mtandao mapema Jana kwenye makao makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.
Alisema kuwa mjadala huo unahitajika Sana kuweza kusaidia kuongeza mapambano hayo kwani kumekuwa na nchi ambazo zimeshindwa kuhoji suala hilo la kupata fedha za kupambana na athari za mabadiliko ya Tabianchi duniani kwa Sasa.
“Tunawezaje kuwalazimisha wanaotoa fedha kutoa kwa wakati kama walivyoahidi kwenye mikataba ya kupambana na athari ya uharibifu wa Tabianchi kote duniani pasi na kuwa na mjadala wa kina wa kuzungumzia suala hilo ili kufikia muafaka wa mikataba hiyo”
“Tunapozungumzia mabadiliko ya Tabianchi sio kwa kipindi kimoja tunahitajika tuyazungumze kwa kina kila Mara kwani kumekuwa na athari kwa nchi zetu huku fedha na vifaa ikiwa ni changamoto kubwa kwa nchi zetu” alisema Lemoyan
Alisema kuwa masuala ya mazingira hayahitaji subra kuyazungumza kwa yamekuwa yakileta athari mbalimbali miongoni mwa jamii zetu ikiwemo majanga ya mafuriko ifike mahali tuwe na Kitengo Cha maafa kwa nchi zetu za Eac.
Akabainisha kuwa nchi zetu kiwango Cha uharibifu wa mazingira ni asilimia 25 na tunahitaji kuwa na usalama wa chakula huku mabadiliko ya Tabianchi yakiendelea kutuathiri utaona jinsi hivyo tukiwa na mfuko wa pamoja wa majanga utasaidia kuomba fedha pamoja na kujichanga ili kukabiliana na suala hilo la usalama wa chakula kwa nchi zetu.
“Uwepo wa mikakati mbalimbali ya pamoja wa kuweka viashiria vya majanga kwa pamoja kwani Utakuta Janga linaanzia nchini Kenya linaishia Rombo nchini Tanzania ifike mahali tukazungumza kwa Umoja wetu jinsi ya kuangalia namna nzuri ya kukabiliana na athari hizo”
Wakichangia mjadala huo wabunge kutoka nchini Burundi walienda mbali na kutaka kuundwa kwa mfuko wa pamoja kwa nchi za Jumuiya hiyo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwenye Ukanda huo.
Walisema mfano nchi hiyo imekuwa na muingiliano ya kimipaka mfano Ziwa Tanganyika hivyo kutaka Juhudi za pamoja za kupambana na athari za mabadiliko hayo kwa umoja wao.
Walibainisha kuwa miradi mingi ya Utekelezaji wa athari za mabadiliko ya Tabianchi fedha zake zinatoka kwenye nchi zenye kuharibu mazingira kwa kiwango kikubwa hususani nchi za magharibi hivyo mpango wa pamoja ikiwemo mijadala kwenye mikutano yao inahitaji kwa kipindi hiki.
Burundi imeridhia itifaki ya mikataba sita ya masuala ya athari za mabadiliko ya Tabianchi na haipo nyuma Sana kwenye utekelezaji wake imeonyesha jinsi athari hizo kwenye sekta ya Kilimo Rasilimali za maji huku ikizitaka nchi za Eac kuhamasisha wananchi kupanda mbegu zenye kuhimili mvua kidogo kutokana na athari hizo za Tabianchi.
Nao wajumbe kutoka Sudani kusini ambao nchi yao bado ni mwanacha mchanga ambaye bado mifumo ya kitaasisi ni changamoto ikiwemo bajeti na wataalamu kwa kuwa inajenga nchi yao Ila sera na mifumo inangojea kupitishwa na Serikali siku zijazo huku ikiridhia itifaki hizo.
Walisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na mashirika ya kimataifa katika kuona wanakabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwani wamekuwa na changamoto ya vifaa vya kupima hali ya hewa kutokana na uchanga wa nchi yao.
Walieleza kuwa wananchi bado hawajahusishwa kwenye masuala ya kiuchumi ambayo yanaleta mabadiliko ya Tabianchi huku udhibiti wa makampuni ya mafuta na madini ndani ya nchi hiyo ukiwa bado ni changamoto ya uharibifu wa mabadiliko ya Tabianchi
Wajumbe kutoka Rwanda walisema kuwa nchi hiyo inazo Taasisi zinazojihusisha na udhibiti wa masuala ya mabadiliko ya Tabianchi lakini changamoto yao ni kilimo Cha kienyeji ambacho limekuwa kikileta athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Pia wamekuwa na tatizo la uwekezaji katika Kitengo Cha udhibiti wa masuala ya Tabianchi,ikiwemo ukosefu wa fedha za ndani kukabiliana kwa kuwa nchi hiyo Ina milima na mabonde hali inayotatiza nchi hiyo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Mjadala huo ulioendeshwa kwa njia ya Tehama kwa wajumbe wa nchi Tatu za Rwanda,Burundi na Sudani ya Kusini kueleza jinsi athari za mabadiliko ya Tabianchi kwenye nchi zao unatarajiwa kuendelea kwa nchi za Tanzania,Kenya na Uganda kueleza changamoto na mafanikio kwa nchi zao kwenye kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi na mikakati yao siku ya kesho.