Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza mara baada ya kukagua shamba darasa la malisho bora ya mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida
Muonekano wa shamba darasa la malisho bora ya mifugo lililopo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mbegu za moja ya aina ya malisho alipotembelea shamba darasa la malisho Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida
Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Angello Mwilawa (kushoto) na Afisa Mifugo Mkuu Bibi Bezia Rwongezibwa wote kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakionesha malisho ya mifugo ambayo yamevunwa tayari kwa kuhifadhiwa.
********************************
Na. Edward Kondela
Serikali imesema itahakikisha changamoto ya malisho ya mifugo nchini inatatuliwa kwa wafugaji kuelimishwa namna ya kulima malisho bora yenye tija kwa mifugo yao.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akikagua shamba darasa la malisho ya mifugo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida na kubainisha kuwa, serikali itaendelea kuwatia moyo wafugaji ili wawe na mashamba ya malisho bora ya mifugo yao pamoja na kuhakikisha uwepo wa maji ya kutosha ya kunyweshea mifugo mambo ambayo yatasaidia kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumaji wengine wa ardhi.
“Makatibu tawala wa mikoa mingine waige mfano wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa mashamba ya malisho ya mifugo, lazima iendelezwe kwenye mikoa mingine. Wafugaji wengine nchini wakiweza kutenga maeneo yao na kupewa mafunzo na kulima malisho yao itakuwa njia sahihi pia ya kuwasaidia wafugaji kuondokana na hali ya kuhamahama ya mifugo yao kutafuta malisho.” Amesema Prof. Gabriel
Aidha Prof. Gabriel ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa kuhakikisha anashirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kutunza mashamba hayo dhidi ya uvamizi wowote wa watu kukata malisho hayo au kuingiza mifugo yao kulisha bila utaratibu unaokubalika.
Pia amewataka wafugaji kote nchini kufahamu nchi yeyote duniani inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi haitamtetea mfugaji yeyote atakayeenda kinyume na sheria kwa kulisha mifugo yake katika eneo au shamba la mmiliki mwingine bila kufuata utaratibu.
Katibu mkuu huyo ameongeza kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha uwepo wa mifugo bora nchini ambayo inatokana na kula malisho bora ya kisayansi, ambapo badala ya kula wingi wa majani wale majani yaliyo bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bw. Justice Kijazi ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kusambaza wataalam wake wa malisho katika maeneo mengine hapa nchini ili kuwashauri wakulima kuwa na mashamba mengi ya malisho bora ya mifugo ambayo yatakuwa na tija kwa wafugaji kwa kuwa na mifugo bora.
Bw. Kijazi amefafanua pia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ina majosho 10 ya kuoshea mifugo huku akiishukuru wizara kwa kuwapatia fedha ya kukarabati majosho matatu na kuiomba wizara iwasaidie pia fedha nyingine kwa ajili ya kukarabari majosho saba yaliyobaki ili wafugaji wengi zaidi katika halmashauri hiyo waweze kuogesha mifugo yao.
Kuhusu idadi ya mifugo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Kijazi amesema kuna jumla ya mifugo takriban 600,000 ambapo ng’ombe wapo 350,000 mbuzi na kondoo zaidi ya 200,000 licha ya halmashauri kuwa na changamoto ya kutokuwa na machinjio nzuri, ameiomba wizara kutoa msaada wowote ili kuiwezesha halmashauri hiyo kuwa na machinjio nzuri na kisasa kulingana na idadi ya mifugo iliyopo na hatimaye kuweza kuuza nyama ndani na nje ya nchi.
Akibainisha umuhimu wa uwepo wa mashamba bora ya malisho yanayotokana na kupandwa kwa aina mbalimbali za nyasi zilizofanyiwa utafiti wa kisanyansi na kuthibitishwa kuwa ni bora kwa malisho ya mifugo, Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bibi Bezia Rwongezibwa amesema wafugaji wanafundishwa kulima, kupalilia, kuweka mbolea, kuvuna na hatimaye kuhifadhi malisho hayo ambayo yatatumika wakati wa uhaba wa malisho.
Nao baadhi ya wananchi wakiwemo wa vikundi vya wajasiriamali ambao wamejitolea kulima mashamba darasa kwa ajili ya mifugo kutoka katika Kijiji cha Mahambe Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, wamesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewatia moyo namna ya kulima malisho na kuyahifadhi ambapo baadhi yao wameanza kupanda malisho hayo ili wapate mifugo bora wakiwemo ng’ombe.
Wamesema uwepo wa mashamba darasa katika eneo lao ni darasa tosha kwao kwa kuwa wataweza kujifunza zaidi kuhusu malisho bora ya mifugo na hatimaye kulima katika mashamba yao.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, wakati akikagua shamba darasa la malisho ya mifugo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, amezungumzia pia kuhusu uwepo wa virusi vya corona nchini vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 ambapo amebainisha kuwa kwenye sekta ya mifugo wizara imeweka mkazo mkubwa kwa jamii ya wafugaji kote nchini kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kukabiliana na janga hilo kwa kuchukua tahadhari, kufanya maombi pamoja na kufanya kazi kwa bidii.