Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare (kushoto) akipokea msaada wa shilingi milioni moja kutoka kwa mwakilishi wa Viongozi wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania Mkoani Morogoro Askofu Brayson Msuya ambaye pia ni Mwenyekiti wa CPCT Morogoro (picha – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa)
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (wa kwanza kulia) akiwa amekabidhiwa fedha na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro zilizotolewa msaada na viongozi wa CPCT kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa CORONA. wa pili kulia ni Katibu wa CPCT Lameck Ngenzi ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Free Pentekoste
*******************************
Na Farida Saidy,Morogoro
Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania (CPCT) Mkoa wa Morogoro wameungana na jitihada za Serikali ya Mkoa huo kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni moja za kitanzania ikiwa ni mchango wao katika kupambana na ugonjwa wa CORONA Mkoani humo.
Viongozi wa CPCT wametoa msaada huo wa fedha mwishoni mwa wiki hii walipofika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kumkabidhi fedha hizo Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare kama ishara ya kumuunga Mkono na Serikali ngazi ya Mkoa katika kupambana na ugonjwa wa CORONA Mkoani humo.
Wakizungumzia mara baada ya kutoa msaada huo, Viongozi wa CPCT wakiongozwa na Askofu Bryson Msuya Askofu wa TAG Morogoro Kaskazini ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CPCT Mkoa wa Morogoro walieleza kuwa wameguswa na jitihada za Mkuu wa Mkoa za kupambana na ugonjwa wa CORONA.
Hamasa ya viongozi hao inatokana na wito alioutoa Mkuu wa Mkoa huo Loata Sanare Aprili 21 mwaka huu katika kikao chake na wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoani humo kilichofanyika katika Chuo cha ualimu cha Morogoro ambapo kwa pamoja walikubaliana kuunganisha nguvu zao ili kupambana na janga la CORONA ambalo bado ni tishio kwa Taifa la Tanzania na Dunia kwa jumla.
Akipokea mchango huo Loata Ole Sanare aliwashukuru viongozi hao kwa mchango walioutoa huku akisisitiza kauli yake anayoitoa mara kwa mara kuwa pamoja na michango ambayo ni muhimu, kubwa aliwataka viongozi hao kutoa elimu kwa watu wanaowahudumia katika maeneo yao namna ya kujikinga na maambukizi ya CORONA.
Aprili 24 mwaka huu yaani siku tatu baada ya kikao cha Mkuu wa Mkoa na wadau kufanyika, michango mbalimbali ilianza kumiminika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kutoka kwa wadau ikiwa ni utekelezaji wa ahadi walizotoa siku ya kikao ambapo siku hiyo pekee vifaa na fedha taslimu vilipatikana, vyote vikiwa na jumla ya zaidi ya shilingi 141Mil.