Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya alisema kuwa Wanapendekeza aina tatu za mchanganyiko wa mimea tiba kutengeneza joto tiba au mvuke kwaajili ya kujifukiza kuondokana na virusi vya magonjwa mbalimbali ikiwemo hili la virusi vya Corona.
Aliutaja aina ya kwanza ya mchanganyiko wa mimea ambayo wananchi wanaweza kuutumia ni mchanganyiko wa majani ya mkaratusi, majani ya kivumbasi au kashwagala na majani ya mchaichai.
Aina ya pili ni mchanganyiko wa majani ya mchaichai, karafuu, tangawizi iliopondwapondwa na majani ya mlimao. Aliutaja aina ya tatu ni kuwa ni mchanganyiko wa majani ya mwarobaini, majani ya mpera, mchaichai na majani ya mlimao.
Kwa mujibu wake, tiba joto hiyo au mvuke ni muhimu kwani inasaidia kuongeza kinga ya mwili, kufungua njia ya hewa na kukirarua kirusi cha corona kama bado kiko kwenye njia ya hewa na hakijaingia kwenye mapafu.
Alisema tiba ya kujifukiza haisaidii kama tayari kirusi cha corona kimeshaingia kwenye mapafu, hivyo mgonjwa anatakiwa kupewa matibabu mengine ikiwemo antibiotic.
Prof.Mgaya alishauri mvuke huo unahitaji Joto la nyuzi 50-70. Anasema “Joto la mvuke linatakiwa liwe kati ya nyuzi 50 hadi 70, likizidi linaweza kuumiza njia ya hewa, mtu anatakiwa avute mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni, watu wazima wavute kwa dakika nane hadi kumi na watoto kuanzia umri wa miaka saba wavute kwa dakika mbili hadi nne, watoto chini ya miaka saba hawaruhusiwi kutumia tiba hii,” alisema Profesa Mgaya.
Kwa kuwa mvuke una kiasi kidogo cha hewa ya oksijeni, alisema watu wenye matatizo ya kupumua hawapaswi kutumia tiba hiyo kwani wanaweza kupoteza maisha, pia wanaotumia wasijifukize wakati sufuria iko kwenye jiko la mkaa bali iwekwe chini au mahali pengine kwa kuwa mkaa hutoa hewa yenye sumu hatari kwa binadamu.
Kuhusu maandalizi ya dawa hiyo, Profesa Mgaya alisema hatua ya kwanza ni kuchemsha maji ya lita tano au kumi hadi yachemke, kisha yawekwe majani na kuyafunika na kuyachemsha kwa dakika tano tu.
Alisema dawa ikichemshwa kwa zaidi ya dakika tano inakuwa imepikwa na haifai kwa tiba kwa sababu virutubisho muhimu vinakuwa vimepotea kwa njia ya mvuke.
Alisema wakati wa kujifukiza mtu anaweza kujifunika kwa blanketi au shuka au taulo zito ili mvuke usipotee, na baada ya kujifukiza muhusika asipewe maji baridi ya kunywa kwani ataharibu tiba bali apewe glasi ya maji ya moto au chai.
Kuhusu kipimo cha dawa hizo, alitoa kipimo kwa mchanganyiko wa kwanza tu ambapo mtu anatakiwa atumie gramu 50 za majani ya mkaratusi na gramu 50 za kivumbasi na gramu 20 za mchaichai.