……………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
WAKULIMA nchini wametakiwa watumie soko la Afrika Mashariki kwa kulima kilimo chenye tija na kutumia teknolojia mpya za kisasa huku wakiaswa kuachana na kilimo cha mazoea cha kujikimu ambacho hakiwaletei faida.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkurugenzi wa shamba darasa lililopo wilaya Kibaha mkoani Pwani Ephrahim Masawe na kuongeza kuwa soko hilo ndilo litakaloinua uchumi wao kwani linafaida kubwa.
Jambo kubwa ni kutumia mbegu bora na kutumia teknolojia mpya ikiwemo ya matumizi ya mbolea inayotokana na maganda ya korosho kwa kuweka kwenye migomba.
Masawe alitaja teknolojia nyingine ni matumizi ya mabaki yanayotokana na uchakataji wa gesi itokanayo na kinyesi cha ngombe bio gas.
“;Teknolojia hizi ni nzuri sana kwani hazina athari za mazingira na hazina gharama kubwa kutokana na kupatikana kwa urahisi hasa kwa wale wanaofuga ngombe na wanaolima zao la korosho,” alisema Masawe.
Aidha aliwataka wakulima kutumia eneo moja kwa kulima mazao mchanganyiko ili kuboresha biashara pamoja na chakula pia hurutubisha ardhi.
Wakulima lazima wajikite kwenye teknolojia mpya za kilimo biashara ili kiwainue kimaisha kuliko kulima kilimo kisicho na tija ambacho hakuna faida na kimepitwa na wakati,”alieleza Masawe.
Masawe aliwaasa wakulima hasa vijana wajifunze kilimo biashara ili kupata utaalamu wa kilimo na ufugaji na kuacha kucheza pool au kukaa vijiweni.