Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa tai) akipata maelezo ya aina za mbegu bora ya pamba zilizogunduliwa na Kituo cha TARI Ukiriguru mkoa wa Mwanza leo.
Watumishi wa chuo cha Kilimo MATI Ukiriguru wilaya ya Misungwi wakimsikiliza Katibu Mkuu ( hayupo pichani) leo alipowatembelea kuzungumza nao.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kushoto) akiwa ameshika muhogo bora unaozalishwa na kituo cha Utafiti wa Kilimo ( TARI) Ukiriguru wakati alipofanya ziara ya kikazi.
*************************************
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo cha Ukiriguru mkoani Mwanza imefanikiwa
kugundua aina kumi za mbegu bora za zao la pamba kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima nchini.
Hayo yamebainishwa leo (30.04.2020) na Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Geofrey Mkamilo wakati
akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo alipotembelea kituo hicho
wilayani Misungwi.
Aina mpya za mbegu zilizogunduliwa ni pamoja na UK 173,uk 08,UK 171 na UK91. Imeelezwa kuwa
mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno tani 2.5 hadi 3.0 kwa hekta na kuwa na zinahimili ukinzani wa
mnyauko fuzari.
Akizungumzia mafanikio hayo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo alisema wizara inataka kuona mbegu hizo
bora zinafikishwa kwa wakulima wote kwenye mikoa 17 inayozalisha pamba nchini.
Aliongeza kusema watafiti wa mbegu bora wanapaswa kuendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais
Dkt.John Pombe Magufuli la kuzalisha mbegu nyingi za pamba na mazao mengine ili nchi ijitosheleze
kwa mbegu.
“ Mikoa 17 nchini inalima zao la pamba na inataka mbegu bora toka Ukiriguru.Tunahijati mzalishe mbegu nyingi zaidi na kusambaza kwa wakulima kwa wakati” alisisitiza Kusaya.
Takwimu za uzalishaji pamba msimu wa 2019 ilikuwa tani 348,910 kati ya lengo tani 450,000 ambazo ziliuzwa kupitia vyama vya ushirika(AMCOS) na kuingiza shilingi Bilioni 419.
TARI Ukiriguru imefanikiwa pia kugundua aina 16 za mbegu za mihogo aina ya Mkumba,Mkuranga
1,Kizimbani,Kiroba,TARICASSA1,2,3,4 na TARICASS 5 zenye uwezo wa kutoa mavuno mengi tani 20
hadi 40 kwa hektari na zenye ukinzani wa magonjwa ya CMD na CBSD.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo ameviagiza Vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini kuanzisha
mashamba darasa bora ya mazao ili wazalishe na kuuza kwa wakulima lengo ikiwa vijiendesha
kibiashara.
Akizungumza na watumishi wa Chuo cha Kilimo ( MATI) Ukiruguru, Katibu Mkuu huyo alisema uwepo wa
maeneo makubwa ya ardhi kwenye vyuo vya mafunzo utumike kuzalisha mazao mengi ya aina tofauti
na kuuza kwenye masoko.
“ Nataka tuone namna vyuo vyetu vitaendeshwa kibiashara kwani uwezo tunao na utaalam upo .Kama
mnaweza kufundisha vijana kilimo cha kisasa na ufugaji kwanini msianzishe kilimobiashara hapa na
kujiongezea kipato ? alihoji Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu huyo amesema wizara inazo taasisi za utafiti wa mazao kama TARI na ASA ambazo
zinajukumu la kuzalisha mbegu ,hivyo vyuo vifanye utaratibu kuanzisha mashamba ya kilimo biashara.
Kusaya ameahidi kupatia chuo cha MATI Ukiruguru trekta moja na kompyuta kumi (10) ili kusaidia
utendaji kazi wa chuo hicho na kuongeza kuwa kuanzia sasa watumishi wote watalipwa stahili za posho
ya masaa ya ziada toka wizarani ili kuinua ari na motisha ya kufanya kazi kwa watumishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Frenk Onesmo alisema wanaendelea na mafunzo ya vijana
katika fani za kilimo na sasa wameanza kufundisha kilimo cha mazao kama alizeti,mdarasini na
mbogamboga ili kuwajengea uwezo.