Wachimbaji madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambapo Takukuru imefanikisha migodi 14 isifutiwe leseni kwa kuhakikisha shilingi milioni 14.5 zinalipiwa.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Manyara, imewasaidia wamiliki wa migodi 14 wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro waliokuwa wafutiwe leseni zao kwa kudaiwa shilingi milioni 14.5 na Wizara ya Madini.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Isdory Kyando wamiliki hao 14 wa migodi walikuwa wanyang’anywe migodi hiyo kwa kutolipa ada za leseni zao.
Kyando alisema leseni hizo zilizopo kitalu B (Opec) zilikuwa zifutwe kwa wanachama hao wa chama cha ushirika cha Mirerani and Naisinyai Small Miners Primary Cooperative Society (Minasco) waliokuwa wanadaiwa fedha hizo.
Alisema awali chama hicho chenye wanachama 50 kilikuwa kinawadai baadhi ya wanachama wake shilingi milioni 58 tangu mwaka 2018, ambayo ni asilimia tano ya mapato ya madini.
Alisema Takukuru wilaya ya Simanjiro iliingilia kati katika kudai fedha hizo ambapo ilikusanya shilingi milioni 19 na kufungua akaunti maalum ili zikikamilika zikabidhiwe kwenye chama hicho cha ushirika.
“Huu ni utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli ya kusimamia urejeshaji wa fedha za vyama vya ushirika sasa miongoni mwa vyama hivyo ni hii Minasco ambayo tuliingilia kati na kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo,” alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa kwa mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika wa Manyara ya wachimbaji hao kudaiwa shilingi milioni 14.5 za ada za leseni waliingilia kati ili kuwanusuru ili wasifutiwe leseni.
Alisema kutokana na mazingira hayo waliona ni busara kuwakabidhi fedha hizo na kusimamia kuhakikisha zinakwenda kulipa deni la leseni ili wachimbaji hao wadogo waendelee kufanya kazi shughuli zao za kila siku” alisema Kyando.
Alisema endapo Takukuru wasingeingilia kati na kusimamia urejeshwaji wa fedha hizo leseni za wachimbaji hao zingefutwa na wengi wao wangekosa ajira.
Alitoa wito kwa uongozi wa Minasco kusimamia mchango wa vyanzo vya mapato kwa umakini na kuhakikisha fedha zisikae mikononi mwa watu binafsi bila sababu za msingi na kuwa na mfumo thabiti wa ulipwaji fedha zao.
Alisema kwa wanachama wa vyama vya ushirika wakiwemo Minasco wahakikishe wanafanya wajibu wao kwa chama, wahakikishe wanafanya marejesho kwa wakati, wahakikishe wanaandaa mfumo mzuri wa kuhifadhi fedha za chama kwani siyo shamba la bibi.