Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi (kulia) akipokea msaada wa simtank 60 kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kuuza magogo ya Gwihaya, Leonard Mahende (kushoto) iliyoko Mafinga mkoani Iringa
………………………………………………………………………………………..
NA DENIS MLOWE,IRINGA
MKUU wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi amelitaka jeshi la polisi kwa kushirikiana na afisa biashara wa mkoa kufanya msako mkali kwa wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari na kuwa kinyume na bei elekezi iliyotolewa na serikali.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vitu mbalimbali vya kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona vilivyotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo juzi, Hapi alisema kuwa kuna wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipandisha bei na kwenda tofauti na bei elekezi.
Alisema kuwa serikali ilitangaza bei elekezi ya sukari hivyo msako huo ufanyike kuweza kuwabaini wafanyabiashara hao kwa kuwa wanaenda kinyume na kauli ya serikali ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwatetea wananchi wake kuondokana na kupandishwa kwa bei ya bidhaa.
Alisema kuwa mara kwa mara kikifika kipindi cha mfungo wa ramadhani wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei ya bidhaa mbalimbali hali ambayo serikali haiwezi kukubaliana nalo kwani hali ya sukari iko salama kabisa nchini tofauti na wafanyabiashara wanavyofanya.
Akizungumzia msaada aliotolewa na wadau wa maendeleo mkoani hapa wakiongozwa na Kampuni ya Asas, Kampuni ya Qwihaya, Sai Energy na Taasisi ya Cliton Foundation ambao wametoa misaada ya Barakoa, dawa na vifaa tiba,nguo maalum za madaktari na waaguzi. Sabuni za maji, tanki za kunawia , themoscanner na vitakasa mikono.
Alisema kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kupambana na maambukizi ya virus vya corona mkoani hapa na kuwashakuru kwa kuweza kuvitoa kwa wakati mwafaka ambapo dunia inapambana kuweza kutokomeza virusi hivyo.
Alisema kuwa katika kupambana na virusi hivyo wananchi wanatakiwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kuwataka ofisi za serikali zote mkoani hapa kuvaa barakao, kunawa mikono na vitakasa mkono na kutowahudumia wananchi ambao hawajavaa barakao hadi wavae.
Alisema kuwa kila taasisi, na ofisi za watu binafsi wazingatie maagizo ya serikali kwa kuweka vifaa vya usafi na sehemu za starehe kuwe na utaratibu maalum kwa wateja wao na kuacha kuwa na mikusanyiko usiyo na maana.
Aidha Hapi aliwataka watendaji kuwafatilia walimu na wazazi ambao wameanzisha masomo kwa watoto majumbani na kufanya mikusanyiko iliyokatazwa na serikali na Latra na vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia uvaaji wa barakao na unawaji wa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka katika vyombo vya usafiri, mabaa na hoteli.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya Qwihaya inayojishughulisha na uuzaji wa magogo yenye makao makuu wilaya ya Mufindi, Leonard Mahende alisema kuwa baada ya janga la Corona kampuni hiyo imewiwa na kuweza kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. Milioni 10.
Alivitaja vitu vilivyotolewa na kampuni hiyo kuwa ni simtank 60 zenye ujazo wa lita 250,vitakasa mikono, mavazi maalum kwa ajili ya matabibu, sabuni za maji, thermometer na lengo la msaada ni kuweza kusaidia wananchi na wauguzi waweze kutuhudumia kwa usalama zaidi.
Aidha alitoa msaada wa vitakasa mikono kwa wanahabari wa mkoa wa Iringa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhabarisha umma juu ya masuala mbalimbali lakini wakisaulika katika mambo mengi ya kijamii.