Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akingea na watumishi wa Bodi ya Pamba nchini ambapo amewataka kubuni mikakati mipya ya kuongeza uzalishaji wa pamba nchini ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya kuongeza thamani ya zao hilo.Tukio hili limefanyika leo jijini Mwanza
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (aliyevaa tai) akiongea na Menejiment ya Chama Kikuu cha Ushirika Mwanza (Nyanza) na kuwataka kujitegemea kimapato kwa kutumia rasilimali za wakulima zilizopo.Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Nyanza Benjamin Mikomangwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akizungumza na watumishi wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) ambapo amekitaka chama kikuu hicho kuhakikisha kinarejesha mali zote zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha utaratibu kama nyumba na mashamba.
*******************************
Mwanza.
Wizara ya Kilimo imekiagiza Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Mwanza (Nyanza) kubuni njia muafaka za
kujitegemea kiundeshaji kwa kutumia rasilimali nyingi ilizonazo.
Agizo hilo limetolewa leo(30.04.2020) Jijini Mwanza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya
wakati alipofanya kikao na watumishi wa chama hicho na kuelezea kusikitishwa kwake na hali ya
utendaji wa chama hicho kushindwa kujiendesha.
“ Tunataka kuona sasa Nyanza mnakuwa na utendaji unaolenga kujiendesha kibiashara tofauti na
ilivyokuwa zamani ili wakulima wa pamba wanufaike na ushirika kupitia mali zao” alisema Kusaya
Alibainisha kuwa wizara ya Kilimo ina lengo la kuiona Nyanza inasimama yenyewe na ya kisasa
inayojiendesha kibiashara kuwakomboa wakulima wa pamba.
Kusaya alisema Chama Kikuu cha Nyanza kinazo mali nyingi ikiwemo nyumba,maghala na mashamba
ambayo kwa sasa hazitumiki kuzalisha mali kwa faida na kuwa zingine bado zinamilikwa isivyo halali na
baadhi ya watu na kutaka ripoti ya mali hizo ipelekwe wizarani kwake ifikiapo Mei 15 mwaka huu.
“ Watieni moyo wana ushirika ili wawe na imani na Nyanza.Nataka nione mkijitegemea na kuwa leo
nilitegemea kusika ripoti ya mafanikio badala ya kunieleza matatizo ya madeni” alisema.
Aidha aliagiza kuwa agizo la Waziria Mkuu kuhusu urejeshwaji wa nyumba nane (8) zilizokuwa
zikimilikiwa isivyo na watu binafsi litekelezwa kwa nyumba hizo kuwa na hati miliki za umma.
Kwa uande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Nyanza Martha Ndeto alisema tayari nyumba saba(7) zilizokuwa zikimilikiwa kinyume ya utaratibu zimerejeshwa na hati zake zipo kwa Msajili wa Ardhi na kuwa kazi inaendelea kufuatilia moja iliyobaki.
Ndeto aliongeza kusema Nyanza kwa sasa inakabiliwa na madeni makubwa yanayofikia shilingi Bilioni 4.23 toka wa mabenki,taasisi za serikali na wafanyabiashara.
Katika hatua nyingine Katibu mkuu Kusaya alitembelea Bodi ya Pamba yenye makao makuu yake jijini
Mwanza na kuagiza kuwa waongeze malengo ya uzalishaji pamba kutoka tani 450,000 za sasa hadi tani
700,000 mwaka ujao.
Alisema amesikitishwa kuona viwanda vya kuchambua pamba kwenye mikoa ya Shinyanga,Simiyu na
Mwanza vinashindwa kufanya kazi mwaka mzima kutokana na upungufu wa malighafi.
“ Nia yangu nikiwa Mtendaji Mkuu wa Wizara ya Kilimo ni kuona uzalishaji wa pamba unaongezeka ili
viwanda vipate malighafi ya kutosha na wakulima wapate fedha za kutosha “ alisisitiza Katibu Mkuu
huyo.
Mkurugezi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco Mtunga alisema bodi yake inaendelea na mikakati
ya kuongeza uzalishaji pamba na kukutafuta pembejeo za kutosha ili wakulima wapate mavuno bora
mengi na soko la uhakika.
Katibu Mkuu Kusaya yupo katika ziara ya kikazi mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua maandalizi ya msimu
wa ununuzi wa pamba utakaonza hivi karibuni na kuongeza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya
Wizara yake .