………………………………………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai na wananchi wa Jimbo la Sumve Mkoani Mwanza kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Richard Mganga Ndassa.
Mhe. Ndassa amefariki dunia ghafla leo tarehe 29 Aprili, 2020 Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amesema “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha ghafla cha Mhe. Ndassa, nakumbuka mimi na yeye tulianza pamoja Ubunge mwaka 1995, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Sumve na mimi nikiwa mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki ambalo sasa hivi linaitwa Jimbo la Chato, namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina”
Mhe. Rais Magufuli amemuomba Spika, Mhe. Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu, Wabunge, wananchi wa Sumve pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo cha Mhe. Ndassa.
Amewataka wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
29 Aprili, 2020