*****************************
NA MWAMVUA MWINYI PWANI
JESHI la polisi mkoani Pwani limetangaza msako wa duka kwa duka ,kuwabaini wafanyabiashara ambao wameficha sukari na kuuza kwa bei isiyo elekezi ya sh .2,700 kwa kilo moja ,ambapo ni kinyume cha sheria .
Kutokana na msako huo ulioanza mkoani hapo ,jeshi hilo ,limeshakamata jumla ya kilo 1,037 za sukari pamoja na watuhumiwa saba wanaodaiwa ni wafanyabiashara walioficha sukari hiyo.
Akizungumzia tukio hilo ,kamanda wa polisi mkoani hapo ,Wankyo Nyigesa alieleza kuwa ,msako mkali unafanywa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa walaji kuwa katika baadhi ya maduka katika mkoa huo wameficha sukari na wanauza kwa bei ya sh .3,500 hadi 4,000 kinyume na bei elekezi ya sh .2,700 kwa kilo moja.
Wankyo aliwataja wafanyabiashara wanaodaiwa kukamatwa ni Adinan Hassan (40) akiwa na kilo 112 na Muhidin Haji (27) akiwa na kilo 460.
Wengine ni Rachel Mkumbo (23) akiwa na kilo 19,Kassim Haji (35)kilo 55,Julitha Leornard (55) kilo 55,Omary Ramadhani (19)kilo 40 na Loveness Mlinga (28) .
Aidha Wankyo alibainisha kuwa, watuhumiwa hao ,wanaendelea kuhojiwa na endapo watabainika kuficha sukari ili kupandisha bei isiyo elekezi watafungiwa leseni zao na kufikishwa mahakamani.
Kamanda huyo alieleza kwamba ,operesheni hiyo ni endelevu na atakaekutwa kaficha sukari ama kuuza bidhaa hiyo kwa bei zaidi ya 2,700 atakamatwa na kupokonywa leseni yake.
Kwa upande wa wananchi akiwemo mama lishe Saumu Athuman aliiomba serikali kushughulikia suala la upandaji wa bei ya sukari ili lisiathiri wananchi kwani baadhi ya wafanyabiashara tayari wameanza kupandisha bei kutoka 2,800 hadi 4,000 kwa kilogramu wakidai nao wananunua kwa bei kubwa.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara mkoani Pwani ,Abdala Ndauka alieleza ,wafanyabiashara wakati wakitakiwa kufuata sheria ya bei elekezi ,serikali ingalie namna ya kudhibiti wauzaji wakubwa ambao wanauza bei kubwa ambapo wanasababisha wafanyabiashara wa chini kununua bei kubwa na kupandisha bei madukani .
Aliwataka wafanyabiashara mkoani hapo kuacha kupandisha bei ya bidhaa hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani .
Mwisho