Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe (watatu kushoto) ametoa msaada wa vifaa vya kujikinga na corona vya thamani ya sh1.5 milioni ikiwemo barakoa 500, madumu 10 ya sabuni za maji na ndoo 200 kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo Mjini Babati jana.
*********************************
Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe (CCM) ametoa msaada wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo vyenye thamani ya sh1.5 milioni.
Mahawe akizungumza mjini Babati jana alisema lengo ni kuhakikisha naye ameshiriki kwa namna moja au nyingine katika kupiga vita virusi hivyo ambavyo hivi sasa vimekuwa kero duniani.
Alitaja vifaa hivyo alivyovitoa ni barakoa 500, ndoo 20 za kunawia mikono na madumu 10 ya sabuni za maji zenye ujao wa lita tano kwa kila moja.
Alitoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi wenye kujiweza kushiriki katika mapambano hayo ya kupiga vita maambukizi ya virusi vya corona.
“Tumuunge mkono Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika mapambano haya ya corona,” alisema.
Aliwataka wananchi wa eneo hilo kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Mmoja kati ya wakazi wa mjini Babati, John Darabe alipongeza jitihada za Mahawe katika kutoa msaada wa vifaa kinga vya maambukizi ya virusi vya corona.
“Wabunge wengine waige mfano huu wa Mahawe wa kupambana na corona kwani tatizo hili siyo la mtu mmoja bali ni letu sote hivyo tunapaswa tushiriki,” alisema Darabe.
Muuguzi wa hospitali hiyo ya rufaa ya mkoa wa Manyara, Maria Thomas alisema vifaa hivyo vinawapa moyo wa kuzidi kufanya kazi kwa wakati huu wa janga lililoenea duniani la corona.
“Tunashukuru na tunampongeza mbunge huyu kwa moyo wake wa kujitolea hadi kufanikisha msaada huu wa vifaa kinga ambao umetolewa kwa wakati muafaka,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aliyoitoa hivi karibuni, Manyara ina watu watatu waliokutwa na visa vya maambukizi ya virusi vya corona.