Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyabiashara katika eneo la soko la Mabibo Jijini Dar es Salaam.
Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, akitoa elimu kwa wafanyabiashara katika kituo cha daladala cha feli Jijini Dar es Salaam.
Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na utoaji elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyabiashara katika kituo cha daladala cha feli Jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………….
Na WAMJW- DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetoa wito kwa wananchi kuteketeza Barakoa zao vizuri baada ya kumaliza matumizi yake kisha kuitupa sehemu salama ili kuepusha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Wito huo, ameutoa Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
“Wale ambao mmevaa Barakoa (mask) zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika (disposable mask) , ukumbuke kabla hujaitupa uitoboe ili mtu mwingine asiweze kuiokota na kuisafisha na kuirudisha katika mzunguko jambo litalosaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa Corona” alisema.
Alisema, katika baadhi ya nchi imethibitika kuwa, mgonjwa mmoja wa Corona anaweza kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja hii inatokana na mwingiliano uliopo baina ya watu, hivyo kutoa wito juu ya kuchukua tahadhari kwa hali ya juu.
“Kwa baadhi ya nchi zilizopata maambukizi, inasemekana kuwa, mtu mmoja aliyeambukizwa virusi hivi anauwezo wa kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja” alisema.
Aidha, alisema kuwa, kwa wale ambao wanatumia Barakoa za kitambaa, kuhakikisha wanabadirisha mask hizo kila baada ya masaa manne ili kuepusha kupata magonjwa mengine, huku akisisitiza kuwa, ni muhimu kabla ya kuivaa zifuliwe kwa maji na sabuni kisha ipigwe pasi ili kujiweka salama zaidi dhidi ya magonjwa.
“Kwa wale ambao mnavaa Barakoa (mask) za kitambaa basi mkumbuke kuwa, mask hiyo inatakiwa ivuliwe kila baada ya masaa manne mpaka sita, na hakikisha kuwa, unaifua kwa maji na sabuni, umeinyoosha ili kama kuna virusi humo waweze kufa, usivae barakoa (mask) ambazo ni chafu” alisema
Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, alisisitiza kuwa, wazazi watoe elimu kwa watoto kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuhakikisha wananawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, huku akisisitiza waepuke kuzulula mtaani kuepusha kuokota Barakoa zilizotupwa hovyo bila utaratibu.
Nae Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), amewakumbusha Watanzania kuepuka msongamano katika maeneo yote, huku akisisitiza kuwa, kama hakuna sababu yakutoka nje ni vema watulie majumbani.