Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma akitangaza rasmi kukihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kujiunga na chama cha NCCR-Mageuzi baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge.
………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mbunge wa Rombo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joseph Selasini ametangaza kurudi Chama alichokiasisi cha NCCR Mageuzi mara baada ya bunge kuvunjwa Juni 30 Mwaka huu.
Uamuzi huo ameutoa leo jijini Dodoma ikiwa ni siku moja baada ya kueleza kuwa ametengwa na familia ya kisiasa ya Chama Chake kupitia Group la Whatsup lenye kupokea taarifa muhimu za wabunge ambalo aliondolewa bila ya kupewa taarifa yoyote.
“Siku zote nilipuuza maneno na mizengwe dhidi yangu kwa kuwa niliamini ni changamoto za kisiasa,pamoja na hayo yote April 25 siku ya jumamosi mwaka huu nilitolewa katika kundi la whatsup(group) ambalo ni nyenzo muhimu katika kazi na uongozi shirikishi ndani ya chama changu bila ya taarifa,hii ni sawa na kusema akufukuzae hakwambii toka” amebainisha Mhe.Selasini
Aidha Mhe.Selasini amesema kuwa walipoasisi mageuzi walikuwa wanapigania haki ya kuchagua na kuchaguliwa haki hiyo haipo ndani ya CHADEMA ya sasa badala yake kwa sasa kuna kikundi cha watu kinachoamua nani awe kiongozi na nani asiwe kiongozi, jambo hili linaudhi sana.