Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea wakiwa kwenye chumba cha Mahakama ya wazi kilichopo katika Mahakama ya Rufani Tanzania, Jijini Dar es salaam, kwa ajili kuendeshea mashauri kwa njia ya “Mahakama Mtandao” (kulia) ni Wakili Msomi wa kujitegemea Bw. Clement Kihoko na (kushoto) ni Wakili wa Serikali Mwandamizi Bi. Jenipha Masue.
Kifaa maalumu kinachotumika kuendeshea mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao kilicho andaliwa kwa ajili ya kusikilizia mashauri wakati wa vikao vya Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Picha na Innocent Kansha – Mahakama
*********************************
Na Innocent Kansha na Magreth Kinabo – Mahakama.
Jumla ya mashauri 157 ya madai na jinai yameanza kusikilizwa katika Vikao vya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kuanzia Aprili 27, mwaka huu hadi Mei 15, mwaka huu,
Miongoni mwa mashauri hayo, 55 yanasikilizwa kwa njia ya Mahakama Mtandao “Video Conference” katika vikao vinavyoendelea Mahakama ya Rufani ya Tanzania, iliyopo Jijini Dar es salaam, pamoja na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na Tabora.
Akifafanua, kuhusu mashauri hayo Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Kelvin Mhina alisema “Katika vikao vinavyoendelea kwa njia ya Mahakama Mtandao vitatumia magereza ya Ukonga kwa wafungwa wa kiume na Segerea itakuwa maalum kwa wafungwa wa kike, alisema Mhe Mhina”.
Aidha, kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na Tabora magereza yatakayotumika ni pamoja na gereza la Wilaya Iringa Mjini na Gereza la Wilaya ya Uyuyi aliongeza Mhe, Mhina.
“Mashauri ya jinai yanasikilizwa kwa njia ya Mahakama Mtandao, wakati yale ya madai yanasikilizwa kwa njia ya kawaida. Mashauri haya yanasikilizwa na Majaji tofauti wa Mahakama hiyo,’’ alisisitiza.
Mhe. Mhina aliongeza kuwa mashauri yanasikilizwa kwa njia ya mahakama mtandao ili kupunguza msongamano mahakamani ili kuweza kuepuka mambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.
Mashauri ya jinai yatakayosikiliza kwa njia ya mtandao kwa upande wa Dar es Salaam ni mashurin 32 na Iringa 12 wakati Tabora ina mashauri 11.
Machi 23, mwaka huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, katika taarifa yake aliyoitoa kwa Umma, aliwataka viongozi wote wa Mahakama katika ngazi zote kuonyesha uongozi wa kuwasaidia Watanzania ili waendelea kupata huduma za utoaji haki katika dunia ambayo inapata msusuko mkubwa virusi vya Corona.