…………………………………………………………………………
Na. Dennis Buyekwa
Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Maendelo na Demokrasia (CHADEMA) Mhe. Tundu Lissu.
Katika maombi hayo namba 42 ya mwaka 20019, mlalamikaji alikuwa akiomba ridhaa Mahakama Kuu ili imruhusu kukata rufaa kwa lengo la kupinga uamzi wa kuvuliwa ubunge baada ya kukiuka Kanuni za kudumu za Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutokuhudhuria mfululizo vikao zaidi ya vitatu vya Bunge hilo bila taarifa.
Baada ya kuwasilisha maombi hayo Mawakili wa Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Madai anaeshughulikia Katiba, Uchaguzi na Haki za Binadamu Bi. Alecia Mbuya walipinga vikali ombi hilo kwa kuwasilisha hoja zenye mashiko zilizopelekea Jaji aliyekuwa akisikiliza shauri hilo kukubaliana hoja hizo.
Wakiwasilisha hoja hizo Mawakili wa serikali waliieleza Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa madai ya Mhe. Lissu ni batili na hivyo hayastahili kusikilizwa kwa vile yanakinzana na kifungu 5(2) cha sheria ya Rufani kama ilivyorekebishwa na sheria ya marekebisho ya sheria Na.25 ya mwaka 2002.
Aidha mawakili wa serikali waliieleza Mahakama kuwa upande wa mlalamikaji haukuwa na haki kisheria kupinga uamzi uliotolewa na Mhe. Jaji Matupa wa kumnyima ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya kiutawala uamuzi halali ambao uliishia kwa Mhe. Lissu kupoteza ubunge wake.
Mawakili wa Serikali waliendelea kuieleza Mahakama hiyo kuwa haikuwa sahihi kupinga maauzi ya Jaji Matupa kwa njia ya Rufaa kwa kuwa maamuzi hayo hayakumaliza shauri hilo kama ilivyopaswa kuwa kisheria kwa kuwa shauri hilo liliishia katika mapingamizi ya awali.
Mawakili wa serikali waliendelea kuieleza Mahakama kuwa katika kesi mbalimbali Mahakama ilishaamua kuwa haiwezi kutoa ridhaa ya kukata Rufaa katika shauri ambalo limeishia njiani kama hili hivyo iliamua kulitupilia mbali kwa kuwa maombi haya hayakukidhi vigezo vya kisheria.
Baada ya kusikiliza kwa makini maelezo kutoka pande zote mbili Jaji aliyekuwa akisikiliza shauri hilo Mhe. Yose Mlyambina alikubaliana na hoja zilizotolewa na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia ukweli kuwa maombi hayo hayakukidhi vigezo vya kisheria.
Katika shauri hilo upande wa Serikali uliongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Madai anayeshughulikia Katiba, Uchaguzi na Haki za Binadamu, Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Alecia Mbuya na Wakili wa Serikali Bw. Erigh Lumisha wakati upande wa mlalamikaji uliongonzwa na Wakili wa kujitegemea Bw. Peter Kibatala.
.