**********************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu akiambatana na Kamati ya ulinzi na usalama ya Tarafa wameongoza msako mkali wa kukagua utekelezaji wa bei elekezi ya sukari iliyotolewa na Serikali hivi karibuni.
Gavana Shilatu alipita kwenye maduka ya jumla na ya rejareja kuona namna Wafanyabiashara wanavyouza sukari ambapo kwa bei ya rejareja hawatakiwi kuuza zaidi ya bei ya Tsh. Elfu tatu (3,000/=) kwa kilogram moja na kukuta maduka mengi wametii agizo la Serikali na kuwasihi Wananchi kutoa taarifa mara moja kwa Serikali ya Kijiji au ya kata endapo watabaini ukiukwaji wa bei elekezi ya Serikali.
“Nimepita kwenye maduka na nimejionea utiifu wa Wafanyabiashara wanavyouza sukari. Niwasihi Watendaji kata na vijiji waendeleze msako kwenye maeneo yao na kuwafichua wanaouza Sukari kwa bei ya kulangua. Ni jukumu letu sote kuwatetea Wananchi wetu wasiuziwe sukari kwa bei ya ulanguzi na ole wake Mfanyabiashara atakayekiuka maelekezo ya Serikali tutamchukulia hatua Kali tutakapo mbaini.” Alisisitiza Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Kamati ya ulinzi na usalama ya Tarafa. Serikali imeingilia kati kwa kutoa bei elekezi ya sukari kufuatia Wafanyabiashara wasio waaminifu kutaka kuwalangua Wananchi, jamii inaaswa kuwafichua Walanguzi wanaokiuka maagizo ya Serikali.