Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), pamoja na askari polisi kituo cha polisi Pangani Ilala wakinyoosha mikono, ishara ya kuunga mkono kampeni ya mikono safi, Tanzania salama inayohamasisha kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka
Mratibu mwandamizi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ASP Edith Swebe akieleza jambo mbele ya timu ya uhamasishaji wa elimu juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona katika kituo cha polisi Pangani Ilala
Msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Flavour) Banana Zolo akinawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, ishara ya kuunga mkono kampeni ya kusafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka kama moja ya nyenzo ya kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa abilia na bodaboda katika kituo cha daladala cha Mbezi kwa Msuguli.
Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi akiongea na madereva boda boda wa kituo cha Mbezi mwisho Jijini Dar es Salaam juu ya tahadhari za kuchukua ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
………………………………………………………………….
Na WAMJW- DSM
Mrakibu mwandamizi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ASP Swebe ametoa wito kwa wananchi, hususan Wana Dar es Salaam kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Ameyasema hayo wakati akiwa katika majukumu yake ya ukaguzi wa namna gani kituo cha Polisi Pangani kilichopo Ilala Jijini Dar es Salaam kimechukua hatua ya kukabiliana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
“Tunaendelea kukumbusha Wananchi wa hususan Wanaotoka Jijini Dar es Salaam kunawa mikono na kuchukua hatua zote za tahadhari zinazotakiwa, tunaendelea kusisitiza kila mmoja katika familia yake aendelee kuchukua hatua ambazo Wizara ya Afya inapendekeza” alisema
Kwa upande mwingine, ASP Swebe ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuja na kampeni ya “Mikono safi, Tanzania salama” inayohamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, hali inayoonesha jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi.
“Kwanza nitoe shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa Kampeni inayoendelea ya “Mikono safi, Tanzania salama”, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi” alisema.
Aidha, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kulisaidia Jeshi la polisi vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ikiwemo vitakasa mikono na Barakoa (mask).
Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya Corona endapo vitakuwepo.
Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.