******************************
NA Maggid Mjengwa.
Corona..
Tafakuri Jadidi:
– Kufunga Ilikuwa Rahisi, Kufungua Kunawawesesha Marais
Ndugu zangu,
Nilipata kuandika hapa; ‘ Alipofeli Cyril Ramaphosa’. ilihusu Lockdown. Nilisema, kuwa alifeli kwenye kuwaambia masikini wake wabaki majumbani wakati hawana hata hizo nyumba zenyewe.
Na kwamba, kwa wengine, wana vyumba tu vya kujisitiri lakini hakika ya kula yao ni lazima watoke kwenda kuhemea.
Kwamba viongozi wengi Afrika, kwa kuwaiga wakubwa, wamejikuta wakiingia kwenye mtego wa kuzifunga nchi zao ( Lockdown) bila kuwa na mipango thabiti ya namna ya watakavyowasaidia raia wao wengi wenye hali duni.
Wahenga walisema; Usimuige tembo kwa kila kitu.
Leo Rais Cyril Ramaphosa amekiri hadharani kuwa lockdown iliwatesa wanyonge. Na kwa vile kuna wengi wamekasirishwa, Ramaphosa nae anapata tabu kwenye kufungua. Mei Mosi ametangaza itakuwa siku ya kuanza kufungua.
Ilivyo Afrika, Rais anaweza kwa urahisi kufunga uchumi, lakini unapofungua lazima uwe na maelezo pia kwanini ulifunga na huku unafungua tatizo likiwa bado lipo?
Ikumbukwe, Afrika Kusini ina watu 200, 000 wasio na makazi. Wengi wao wako Johannesburg.
Kufunga nchi kwa maana ya kusimamisha shughuli za kiuchumi ni moja ya hatua za kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya Corona.
Hata hivyo, hatua hiyo inataka umakini mkubwa. Na kuna nchi zimeharakisha kwenda kwenye hatua hiyo na kusababisha athari zaidi kwa watu wake.
Nikaweka bayana, kuwa modeli ya Tanzania bado inafanya kazi na hadi sasa imeepusha athari zaidi za kiuchumi na kijamii. Rais Magufuli alikuwa na ujasiri wa kiuongozi kuliona tatizo la ku- lockdown na kuvumilia shutuma zote.
Inachohitaji Tanzania baada ya kudhibiti viwanja vya ndege, ni kudhibiti mipaka ya nchi kavu na majini na huku ikiongeza elimu ya umma juu ya janga hilo.
Ni Tafakuri Jadidi.