Makatibu Wakuu wakitaza kazi ya ujenzi ghala la kuhifadhia mazao kijiji cha Mbogo Komtongo wilaya ya Mvomelo ambalo muda wake wa ujenzi umeisha lakini halijakamilika.Wa kwanza toka kushoto ni Bw.Gerald Kusaya (Wizara ya Kilimo),Bw.Gerald Mweli(Naibu Katibu Mkuu,OR-Tamisemi na Prof.Riziki Shemdoe ( Katibu Mkuu Viwanda na Biashara) na wa wa kwana kulia ni Mratibu wa Mradi wa ERPP Eng.January Kayumbe
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyeshika kofia) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira Balozi Joseph Sokoine wakikagua mradi wa ujenzi ghala la kuhifadhia mpunga kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomelo jana
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akiongoza kamati ya makatibu wakuu kukagua skimu ya umwagiliaji zao la mpunga katika kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa jana.Uzalishaji katika skimu hiyo umeoanda toka tani 2.5 kwa ekari hadi tani 5.5 za mpunga kwa ekari.
………………………………………………………………………………..
Morogoro.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa onyo kali kwa wakandarasi waliozembea kukamilisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji wilaya ya Mvomero na Kilosa
Kusaya ametoa onyo hilo jana (22.04.2020) wakati alipoongoza ziara ya wajumbe wa kamati ya tendaji ya utekelezaji wa Mradi wa Kuongeza Thamani zao la mpunga ( Extending Rice Production Project-ERPP) katika mkoa wa Morogoro
Makatibu Wakuu wengine walioshiriki ziara hiyo ni Prof.Riziki Shemdoe (Viwanda na Biashara) pia Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine (Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweli (Ofisi ya Rais-Tamisemi)
“ Hatujaridhishwa kabisa na wakandarasi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka ya kijiji cha MbogomKomtonga na Kigugu kwa kutokamilisha kazi ndani ya mkataba ” alisema Kusaya kwa niaba ya kamati hiyo.
Katika hali isiyo ya kawaida kamati ya Makatibu Wakuu ilichukizwa na kitendo cha mkandarasi M/s AMI & VAI Investment ya Dar es Salaam anayejenga ghala la kuhifadhia mpunga kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomelo kwa gharama ya shilingi Milioni 816.37 alikimbia eneo la mradi licha ya kuwa na taarifa za ujio wa makatibu wakuu.
Alipoulizwa alipo mkandarasi wa mradi huo,msimamizi wa mafundi Abdul Kabanika alisema “ Bosi tulikuwa naye hapa muda mfupi uliopita lakini sasa hatumuoni .”
Taarifa zilisema kampuni hiyo ya M/s Ami &Vai Investment imeshindwa kumaliza kazi ndani ya mkataba ulioisha tarehe 21 Aprili 2020 na ujenzi upo asilimia 70 .
“Natoa muda hadi ifikiapo saa 11 jioni leo (Jumatano) mkandarasi M/s AMI & VAI Investment awe amejisalimisha kwangu,kwani ajue serikali ina mkono mrefu.Tutamsaka kotote na kumrejesha hapa Kigugu atueleze kwanini kazi yetu hajakamilisha” alisema Kusaya.
Kamati ilikagua pia mradi wa ghala kijiji cha Mbogo Komtongo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 70 chini ya mkandarasi M/s Shekemu kwa gharama ya Shilingi Milioni 790.87 lakini haujakamilika.
Katibu Mkuu Kusaya alionya na kusema kutokamilika kwa miradi hii kutakua ni kikwazo kwa wakulima kukosa mahala pa kuhifadhi mazao yao na lengo la serikali kutotimia.
Awali kamati hiyo ilitembelea skimu ya umwagiliaji kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa na kujionea hali ya miundombinu kwa ajili ya mashamba ya mpunga ya wakulima iliyofikia asilimia 84 ya ujenzi mitaro na banio.
Skimu hiyo inajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.97 na mkandarasi M/s Whitecity International Ltd akishirikiana na M/s Skyline Properties Ltd na kwa mujibu wa mratibu wa mradi kiasi cha shilingi Milioni 713.15 zimelipwa sawa na asilimia 54.
Alipoulizwa kwanini mradi haujakamilika msimamizi wa mradi huo Mhandisi Emanuel Norbet alisema wamechelewa kukamilisha kutokana na uwepo wa mvua nyingi msimu huu zilizoharibu miundombinu ya barabara na mitaro.
Katika hatua nyingine ,kamati iliridhishwa na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa kwa asilimia 99 lililojengwa na mkandarasi M/s B.H Ladwa Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 971.31 ambapo tayari shilingi milioni 536.06 zimelipwa.
Baada ya ukaguzi wa miradi hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo alisema serikali itahakikisha sheria inachukuliwa ili mkradi ikamilike kwa mujibu wa mikataba.
“Mikataba yote imekwisha,nataka miradi hii iishe na wakulima wapate maji kwa ajili ya kutekeleza kalenda zao za kilimo na serikali ya Rais John Magufuli haitaki wakandarasi wazembe.Tunataka wakulima wapate maji kwenye mitaro ili waendelee na kilimo cha mpunga” alisema Kusaya
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof.Riziki Shemdoe amewaagiza washauri wasimamizi wa miradi hiyo ambayo haijakamilika kuchukua sheria na kuanza kukata fedha kwa wakandarasi wazembe.
“ Hatua za kisheria kukata fedha kwa mujibu wa mkataba zichukuliwe haraka,kwani mikataba imeisha na muda wa nyongeza umeisha.Fedha ya serikali ianze kukatwa kila siku (liqudated damages) “ alisema Prof.Shemdoe
Akizungumza hatua alizochukua msimamizi wa miradi ya ujenzi wa maghala Kigugu na Mbogo Komtonga Architect Ismail Mvungi aliwajuisha wajumbe kuwa tayari wameanza kuwakata wakandarasi hao kiasi cha shilingi 400,00 kila siku kwa kuchelewa kukamilisha kazi.
Mradi wa mradi wa ERPP Mhandisi January Kayumbe alisema miradi hiyo ya ujenzi ilitekelezwa kwa mwaka mmoja na muda wake unamalizika 30 Aprili 21 mwaka huu ,hivyo wakandarasi ambao hawajakamilisha taratibu za sheria zitafuatwa.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigugu kata ya Sungija wilaya ya Mvomelo Damas Mnyani alisema miradi hii itasaidia kuongeza uhakika wa upatikanaji maji kwenye mashamba ya mpunga hali itakayoongeza uhakika wa uzalishaji.
“ Kuwepo kwa skimu hizi kwenye vijiji vyetu kutasaidia kuondoa tishio la njaa kwani tutalima mpunga mwaka mzima na kuhifadhi kwenye maghala tuliyojengewa na serikali yetu.” Mnyani
Mradi huo umefanikiwa hadi sasa kuongeza uzalishaji zao la mpunga toka tani 2.5 kwa ekari hadi tani 5.5 kwa ekari baada ya miundombinu kuboreshwa.
Mradi wa ERPP ulianza kutekelezwa mwaka mwaka 2015 kwa gharama ya Dola za kimarekani milioni 22.91 toka Benki ya Dunia ukijusisha Tanzania Bara na Zanzibar.
Jumla ya miradi 11 ikiwemo ujenzi wa skimu 5 za umwagiliaji,ujenzi wa maghala 5 na ujenzi wa maabara moja ya mbegu inatekelezwa katika mkoa wa Morogoro chini ya ERPP.