Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma (hawapo pichani) wakati akitangaza taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya vyanzo vya ndani vya halmashauri kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020.
……………………………………………………………………..
Na Alex Sonna, DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, amesema katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwenye kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya kiasi cha Sh.Bilioni 126.77 huku Mkoa wa Rukwa ukishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya Sh.Bilioni 6.34.
Aidha, amesema Halmashauri ya Jiji la Dodoma limeongoza kwa makusanyo mengi kiasi cha Sh.Bilioni 36.04 huku Jiji la Dar es salaam likiwa la mwisho ambapo limekusanya Sh.Bilioni 8.83.
Jafo ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapato na matumizi kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020.
Amesema Halmashauri 58 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 75 au zaidi kwa kulinganishwa na makisio kwa mwaka wa fedha 2019/20, Halmashauri 96 zimekusanya asilimia 50 au zaidi lakini chini ya asilimia 75 na Halmashauri 31 zimekusanya chini ya asilimia 50 ya makisio ya mwaka.
Hata hivyo, amesema Mkoa wa Njombe umekusanya wastani wa asilimia 87 ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo huku Mkoa wa Simiyu ukiwa umekusanya wastani wa asilimia 51 kwa kigezo cha asilimia.
Amesema katika kipindi hicho Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kwa kigezo cha asilimia imekusanya kwa asilimia 78 ya makisio yake ya mwaka. na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ya mwisho katika kundi hilo ambapo imekusanya kwa asilimia 55 ya makisio yake ya mwaka.
Aidha, amesema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeongoza kundi hilo kwa kukusanya kwa asilimia 100 ya makisio yake huku Manispaa ya Lindi imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya kwa asilimia 49 kwa kigezo cha asilimia.
Jafo amesema wa Halmashauri za Manispaa ya Manispaa ya Ilala imeongoza kwa kukusanya Sh.Bilioni 43.14 huku Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Sh.Bilioni 1.20
Waziri huyo amesema Halmashauri ya Mji wa Njombe imeongoza kwa kukusanya kwa asilimia 130 huku Halmashauri ya Mji wa Handeni imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43.
Amesema Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa Mapato kwa kukusanya Sh.Bilioni 7.02 huku Halmashauri ya Mji wa Mbulu imekuwa ya mwisho katika kundi hilo ambapo imekusanya Sh. Milioni 671.78.
Amebainisha Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeongoza kwa kukusanya asilimia 126 huku Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imekuwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 30 ya makisio, huku Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya Sh. Bilioni 5.78 huku Gairo imekuwa ya mwisho kwa kukusanya Sh. Milioni 343.7.