Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), akikabidhi boksi la vitakasa mikono (sanitizer) Mrakibu msaidizi wa polisi (ASP) Angelica, makao makao makuu ndogo ya jeshi la polisi, Posta Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akikabidhi vitakasa mikono kwa askari wa jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani ili viwasaidie kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona wakati wa kutoa huduma kwa wananchi, katika eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Lemutuz Brand, vyombo vya utoaji habari za kwa njia ya mtandao, Ndg. Lemutuz akinawa mikono yake kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji kwa wananchi juu ya kunawa mikono, kama moja ya njia ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Afisa kutoka jeshi polisi kitengo chaushrikishaji jamii Stafu Sajenti Valentino Ngowi akiongea na Dereva boda boda na Bajaji, kuhusu elimu ya kujikinga kupata maambukizi ya virusi vya Corona.
Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR na kampuni ya Mjomba Gallery ikiendelea na utoaji elimu kwa wafanyabiashara wa Kariakoo Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Dereva boda boda wa eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam wakisikiliza elimu kuhusu mbinu za kujikinga kupata maambukizi ya virusi vya Corona.
Wakazi wa eneo la Keko Jijini Dar es Salaam wakisikiliza elimu kuhusu mbinu za kujikinga wao na Watoto wao kupata maambukizi ya virusi vya Corona kutoka kwa timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR.
………………………………………………………………
Na WAMJW- DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuwalinda Watoto wao dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuhakikisha wanajikinga vizuri na kuwakinga watoto wao dhidi ya virusi hivyo,
Wito huo ameutoa, Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona
Ndg. Anyitike Mwakitalima amesema kuwa, Watoto wanaweza kuwa chanzo cha kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona katika jamii na familia, hivyo amesisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawadhibiti watoto kuzulula mitaani katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi hivyo.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya inatoa wito ambao inautoa ni kwamba wazazi na walezi tukumbuke kuwalinda watoto wetu, wakae na watulie majumbani kwa kipindi hiki shule zimefunga, msiwaruhusu waende kuzulula maeneo mbali mbali, kwani wanaweza kupata maambukizi huko wanakoenda kucheza” alisema.
Mbali na hayo, alisisitiza kuwa, wazazi watoe elimu kwa watoto kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuhakikisha wananawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, huku akisisitiza waepuke kushika macho, pua na mdomo ili kuzuia kupata maambukizi hayo.
“Wazazi na walezi tuwakumbushe Watoto kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, tuwakumbushe Watoto kuepuka kushika pua, mdomo na macho kwa mikono kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewalinda watoto watoto wetu na tutajilinda sisi wenyewe kupata maambukizi ya virusi vya Corona ” alisema
Kwa upande wake, Afisa kutoka jeshi polisi kitengo chaushrikishaji jamii Stafu Sajenti Valentino Ngowi amewaagiza madereva na makondakta wao kuhakikisha kila siku jioni wanapokuwa wamemaliza kazi zao Kutakasa magari yao kwa dawa maalum aina ya jiki, ili kuua virusi vinavyoweza kuwepo na kupelekea maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Nae Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), amewakumbusha Watanzania kufuata maelekezo ya Wataalamu wa Afya ikiwemo kuepuka msongamano katika maeneo yote, huku akisisitiza kama hakuna sababu yakutoka nje ni watulie majumbani.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha Watanzania kuendelee kufuata maelekezo ya wataalam wa afya, ikiwemo kuepuka misongamano isiyo na ulazima, na kama huna sababu ya kutoka nyumbani ni vyema ukabaki nyumbani” alisema