……………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe amepinga vikali tabia mbaya ya kunyanyapaa Watu wanaokuja toka kwenye maeneo ya wilaya na mikoa mingine kwa kuwahisi wameambukizwa virusi vya Corona pasipo kuthibitishwa na Wataalamu wa afya.
Gavana Shilatu amewasisitiza Wananchi wa Tarafa ya Mihambwe kuzijua vyema dalili za Mtu mwenye virusi vya Corona kama vile kikohozi kibichi, homa, maumivu ya mwili, kuuma kwa koo na awe amethibitishwa na Wataalamu wa afya na sio kuanza ubaguzi wa kunyanyapaana kama njia za kujikinga.
Gavana Shilatu aliwaeleza njia za kujikinga ni kuosha mikono kwa sabuni kwa maji yanayotiririka, kuepuka kugusana, kuepukana mikusanyiko, kuvaa barakoa na si kunyanyapaana.
“Kuchukua tahadhari haimaanishi kuanza dhambi ya ubaguzi ya kunyanyapaana kwa kigezo cha Mtu kutoka kwenye maeneo tofauti, hii si sawa. Nakemea vikali tabia hii, muhimu kujua dalili za ugonjwa wa Covid 19 ambazo mnazijua na tuchukue tahadhari ya kujikinga na virusi vya Corona. Hakuna tahadhali ya kujikinga inayosema tuwanyanyapae Watu, tuache tabia hii.” alisisitiza Gavana Shilatu.
Gavana Shilatu alipita na timu ya Wataalamu wa afya na kutoa elimu ugonjwa wa Covid 19 kwa njia ya matangazo na kuongea na Watu wanaokutana nao njiani kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Tarafa ya Mihambwe.