Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) akitoa ahadi Bungeni ya kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa mafao ya wastaafu wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.
………………………………………………………………..
James K. Mwanamyoto-Dodoma
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imepanga kukutana na Maafisa Utumishi wote nchini ili kuwakumbusha na kuwasisitiza umuhimu wa kuandaa mapema taarifa za mtumishi anayetarajia kustaafu, miezi sita kabla ya kustaafu kwake ili kuondokana na tatizo la ucheleweshwaji wa mafao ya wastaafu ambao baadhi yao hufariki bila kupata mafao yao.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) alipokuwa akitoa ufafanuzi wa namna atakavyotekeleza ahadi aliyoitoa Bungeni ya kuhakikisha ofisi yake inatatua changamoto ya ucheleweshwaji wa mafao ya wastaafu wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.
Mhe. Mkuchika amesema, yeye kama Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora anakwazwa na kitendo cha wastaafu walioitumikia nchi kwa uadilifu kuchelewa kupata mafao yao kwa wakati.
“Nasononeshwa na kitendo cha wastaafu walioitumikia nchi kwa uadilifu na uzalendo kucheleweshewa mafao yao kwa muda mrefu, kuanzia mwaka mmoja hadi minne na wengine kufariki bila kupata mafao yao”, Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe. Mkuchika ameainisha kuwa, katika kipindi cha uongozi wake amebaini kuwa, tatizo la wastaafu kuchelewa kupata mafao linasababishwa na baadhi ya Maafisa Utumishi kuchelewa kuandaa taarifa za wastaafu mapema na kuziwasilisha kwenye mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na kitendo cha baadhi ya waajiri kutowasilisha michango ya watumishi kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewapiga marufuku Maafisa Utumishi kuwaelekeza wastaafu kufuatilia mafao yao jijini Dodoma au Dar es Salaam na badala yake wao ndio wabebe jukumu hilo kwani wastaafu wengi wanapata usumbufu na kukabiliwa changamoto ya ukosefu wa fedha.
Mhe. Mkuchika ametoa rai kwa Maafisa Utumishi kuwajibika ipasavyo na ikitokea mstaafu amechelewa kupata mafao yake, Afisa Utumishi ndiye atatakiwa kuieleza Serikali sababu za mstaafu huyo kutopata mafao yake kwa wakati, ikizingatiwa kuwa Serikali imeshawaelekeza mafisa hao kuhakikisha wanaandaa taarifa za watumishi wanaotarajiwa kustaafu mapema iwezekanavyo.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, Ofisi yake inahusika na Utawala Bora hivyo itahakikisha mstaafu analipwa stahili zake kwa wakati, kitendo cha mstaafu kukaa miaka nne bila kulipwa mafao hakiakisi dhana halisi ya Utawala Bora.
Tatizo la Wastaafu kutopata mafao kwa wakati limekuwa likiwaathiri wastaafu ambao
wanashindwa kufurahia matunda ya Utumishi wao, hivyo Serikali imedhamiria kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa mafao kwa kukutana na Maafisa Utumishi ili kuweka mkakati madhubuti wa kuondokana na tatizo hili.