Mganga mkuu wa Serikali Prof: Muhamad Bakari Kambi wa pili kulia, akipokea vifaa kinga kutoka kwa mwakilishi wa Ubalozi wa Pakistan nchini Tanzania Muhammad Saleem,kwa ajili ya kukabiliana na ugonwa wa Corona nchini.
*************************
Na WAMJW – Dar es Salaam
21/04/2020 Serikali imepongezwa kwa jitihada inazozifanya katika kukabiliana na ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na mwakilishi wa Ubalozi wa Pakistani hapa nchini Muhammad Saleem wakati akikabidhi vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Saleem alisema tangu ugonjwa huo ulipoingia hapa nchini mwezi uliopita kasi ya maambukizi ni ndogo ukilinganisha na nchi zingine, hiyo yote ni kutokana na hatua thabiti zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
“Nchi yetu ya Pakistani imekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania, hivyo basi tumeona nasi tutoe msada wa vifaa kinga. Tunaomba mpokee mchango wetu ambao ni kidogo ili watoa huduma wa afya waweze kutumia vifaa hivi wakati wanawahudumia wagonjwa kwani ugonjwa huu ni janga la Dunia”, alisema Saleem.
Mwakilishi huyo wa Ubalozi wa Pakistani aliishauri Serikali kuendelea kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii katika kutoa elimu ya ugonjwa wa COVID-19 ili wananchi waendelee kupata elimu ya kutosha ambayo itawasaidia kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Serikali Prof. Muhamad Bakari Kambi aliushukuru Ubalozi wa Pakistani kwa msaada walioutoa na kusema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Prof. Kambi alisema ugonjwa wa COVID -19 ni janga la Dunia, watu wengi wamepata madhara kutokana ugonjwa huo hivyo basi hakuna msaada mdogo. “Msaada wowote unaotolewa kwa Serikali utanasaidia kwa kiasi kukubwa katika kukabiliana na ugonjwa”.
Ubalozi wa Pakistani umetoa msaada wa barakoa za upasuaji 1800, kofia ambazo zinavaliwa na wahudumu wa afya wakati wanahudumia wagonjwa 1800, kava za viatu za kuvaliwa wodini 800, barakoa za N95 zipatazo 500, magauni ya kuvaa watoa huduma za afya 100, glovu 8000 pamoja na miwani ya kujikinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona 60. Thamani ya vifaa hivyo ni zaidi ya milioni 11.