*******************************
Na Maggid Mjengwa.
Bado zinasikika kelele za wapiga ving’ora vya hatari ( Alamister) wenye kutaka Serikali itangaze lockdown ya nchi nzima.
Huko nyuma kuna tuliojenga hoja kuwa lockdown ingewaumiza zaidi wanyonge na kwa vile tulishaiona mifano kwa wengine.
Twende leo tukaione Afrika Kusini. Ni mfano wa nchi moja kati ya kadhaa za Kiafrika ambazo Serikali zake ziliharakisha kutangaza lockdown na kuacha raia wake wanyonge kwa mamilioni wakiwa kwenye wakati mgumu.
Juzi hapa, Ijumaa ya Aprili 17, ilipaswa kuwa siku ya mwisho kwa watu wa Afrika Kusini kubaki majumbani. Siku 21 alizotangaza Rais wao, Cyril Ramaphosa za lockdown zilipaswa kuwa zimemalizika.
Lakini, kabla ya Pasaka Ramaphosa aliongeza siku 14 nyingine.
Ilivyo sasa mitaa ya miji ya Afrika Kusini imeanza kujaa tena walalahoi na wengineo waliochoka kufungiwa ndani. Na si kuchoka tu, kwa walalahoi wengi inahusu uhai wao. Wana njaa.
Ili makali ya lockdown yapunguzwe, Waziri wao wa Afya kaweka sharti, kuwa maambukizi mapya yasipozidi 90 kwa siku ndipo ukali utakapopungua.
Kwanini Modeli yetu bado inafanya kazi?
Kuwafungia watu majumbani bila kuwa na mikakati ya kuwasaidia wakiwa majumbani kwa kipindi chote wakiwa ndani ni kutengeneza matatizo mengine, na hata vurugu za kijamii.
Na hili la lockdown lingefanyika, leo hao hao wenye kutaka tuwe na lockdown wangekuwa mstari wa mbele kuwatetea walalahoi kwa hoja za kujaa makapu na hata kufika Mahakamani.
( Angalia mfano wa Malawi).
Tunadhani elimu zaidi iendelee kutolewa juu ya janga hili na masharti mapya yatolewe kila inapojitokeza hali mpya. Mfano hili la sasa la kuzuia watu kunywa baa na kula migahawani.
Onw watu wa Dar Es Salaam wameelekezwa kuanzia leo ( Jumatatu) wavae barakoa na mwitikio umekuwa chanya kwa kiwango cha kushangaza. Njiani nilimopita katika kila watu 10 niliokutana nao 8 walivaa barakoa. Wengine walijifunika mpaka na leso.
Muhimu kwa Serikali ni kuhakikisha bei ya barakoa inashuka. Kwa ruzuku ya Serikali walau zingeuzwa kwa shilingi mia tano kwa moja.
Naam, kubwa kabisa watu waelimishwe ikiwamo kuepuka mikusanyiko na kutokutoka majumbani isipo lazima.
Watanzania bado wana imani na nidhamu ya kusikiliza maelekezo ya wataalamu. Ni kazi ya wataalam hao sasa kutoa elimu na maelekezo bila nchi kulazimika kuwa kwenye hali ya lockdown.