Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiwasili ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kikazi kukagua kukagua athari zilizosababishwa na korongo kubwa kando ya Mto Shaban Robert mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akipewa maelekezo na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Jabir Shekimweri kuhusu namna korongo lililopo katika Mto Shaban Robert linavyoathiri wakazi wa eneo hilo wakati aliponya ziara ya kikazi wilayani humo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia) akiangalia athari za kimazingira zilizosababisha kukatika kwa mawasiliano baada ya daraja la Mto Shaban Robert wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kusombwa na maji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia) akizungumza na wananchi wa Kata ya Mpwapwa Mjini alipofanya ziara ya kikazi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kujionea na kusikiliza changamoto za kimazingira zinazosababishwa na korongo lililopo kwenye Mto Shaban Robert.
Sehemu ya korongo kwenye mto Shaban Robert wilayani Mpwapwa mkoania Dodoma ambalo limeleta athari kwa wananchi wa eneo hilo pindi mvua inaponyesha na kusababisha maji kuzingira makazi.
Sehemu ya nyumba za wakazi wa eneo la Kata ya Mpwapwa Mjijni wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma ikiwa imezingirwa na maji hatua liyosababisha baadhi ya nyumba kubomoka kufuatia korongo lilipo katika Mto Shaban Robert.
…………………………………………………………………..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu mwishoni mwa wiki amefanya ziara ya kikazi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kukagua athari zilizosababishwa na korongo kubwa kando ya Mto Shaban Robert.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo aliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya haraka kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ili kunusuru wananchi kuzingirwa na maji yanayojaa katika mto huo.
Waziri Zungu alisema pamoja na hayo Serikali kupitia Ofisi yake imeichukua changamoto hiyo na kuahidi kukaa na wataalamu wa mazingira kuanza utekelezaji wake.
”Athari hii sio ndogo ni kubwa na inahitaji uangalifu mkubwa katika kuitatua kwani
kila siku maji yanaongezeka katika mto huu, pia sisi kama Serikali tumetenga
fedha za kukabiliana na maafa kama kupitia mifuko ya kitaifa na ya kimataifa
hivyo tutazama tuone nini tunafanya,” alisema.
Aidha Waziri Zungu aliwataka wananchi kuendelea kushiriki katika suala zima la uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti na kuitunza ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa shughuli za binadamu zinachangia kwa kiasi kikubwa kwa matatizo hayo ambayo yamewaletea madhara ikiwemo kukatika kwa mawasiliano baina ya eneo moja hadi lingine baada ya madaraja kusombwa na maji ya mto yaliyofurika isivyo kawaida.
Pia waziri huyo aliwaahidi wananchi kuwasiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma kufahamu wana mkakati gani katika kurudisha mawasiliano ya daraja lililosombwa na maji.
”Ombi langu kwenu muendele kulinda mazingira kwani tukiharibu mazingira
watoto wetu watateseka na dini zote zimesisitiza kulinda mazingira. Pia
tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atunusuru na janga hili la Corona ili
Taifa letu liendelee na shughuli za kawaida na pia tuendelee kujikinga kama
wanavyoelekeza wataalamu wa afya”; alisisitiza.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George Lubeleje aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutenga fedha kiasi cha sh. bilioni 17.4 kwa ajili ya wilaya tano ikiwemo Mpwapwa kutekeleza miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbunge huyo aliwaomba wananchi kuacha kufyeka na kuchoma miti kwa ajili ya mkaa hususan katika maeneo ya milima kwa kuwa hatua hiyo inasababisha kuharibiwa kwa vyanzo ya maji.
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Mpwapwa, Emmanuel Lukumay aliahidi kuwa watafanyia kazi changamoto hiyo kunusuru eneo la korongo kwa kutenga sh. milioni 457 kwa ajili ya kujenga daraja la kudumu.
Lukumay alibainisha kuwa daraja hilo lililojengwa zaidi ya miaka 60 iliyopita na kusombwa na maji hivi karibuni lilikuwa ni kiungo muhimu kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Aliongeza kuwa TARURA daraja liko chini ya mradi wa barabara ya lami iliyoanza kujengwa katika wilaya hiyo na kusema kuwa tayari wameomba fedha kwa ajili ya kulijenga.