Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Renatus Mathias akiongea jana wakati wa mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wauguzi na matatibu kutoka zahanati na vituo vya Afya mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo ikiwa ni mkakati wa Hospitali hiyo kupunguza vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,watoto wachanga na walio chini ya umri wa miaka mitano,katikati Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Wendy Robert na kulia afisa lishe wa wilaya Martha Kibona.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Wendy Robert katikati na Muuguzi Mkuu wa wilaya hiyo Renatus Mathias wa nne kutoka kushoto wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wauguzi waliopata mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya mkakati wa wilaya hiyo katika kupunguza vifo vya mama wajawazito,watoto wachanga na walio chini ya umri wa miaka mitano.
Picha na Mpiga picha wetu
………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
WAUGUZI na matabibu kutoka vituo mbalimbali vya Afya wilayani Tunduru,wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo namna bora ya kuwahudumia mama wajawazito na watoto wachanga na utoaji huduma za dharura za msingi kwa mama wajawazito pindi wanapofikishwa katika vituo vya kutolea huduma.
Katika mafunzo hayo,wauguzi wamefundishwa namna ya uanzishwaji wa Daftari la mama wote wajawazito wenye vidokezo vya hatari wanaopatikana kipindi cha kliniki wanaotakiwa kuelekezwa vidokezo vya vya hatari wakati wote wa ujauzito wao,ambapo viongozi wa serikali za vijiji na watoa huduma ngazi ya jamii ni washiriki na wahusika wakubwa.
Muuguzi Mkuu wa wilaya ya Tunduru Renatus Mathias alieleza kuwa, mafunzo hayo yanakusudia kumaliza vifo vya mama wajawazito wanaofikishwa katika vituo kwa ajili ya kujifungua na hata watoto wachanga na wale walio na umri chini ya miaka mitano.
Alisema, mwaka 2018 vifo vilivyotokana na uzazi kwa mama wajawazito vilikuwa 13 wakati mwaka 2019 vilipungua hadi kufikia 5,hata hivyo mkakati waliojiwekea ni kufikia 0 katika mwaka 2020.
Kwa mujibu wake, mwaka 2018 akina mama wajawazito asilimia 97.6 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma ambapo mwaka 2019 asilimia 99.4 ya akina mama walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma.
Aidha takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2018 asilimia 2.4 ya akina mama wilayani Tunduru,walijifungua katika maeneo yasio ya kutolea huduma za Afya ikiwemo kujifungua kabla ya kufika kituoni,kujifungua kwa wakunga wa jadi na wengine kujifungulia nyumbani tofauti na mwaka 2019 ambapo idadi hiyo ilishuka hadi kufikia asilimia 0.6.
Kwa mujibu wa Renatus, mwaka 2018 watoto wachanga 51 walizaliwa katika vituo vya kutolea huduma na mwaka jana 2019 watoto waliozaliwa katika vituo hivyo walikuwa 42.
Alisema, mtoa huduma ambaye atasababisha kifo cha mama mjamzito au mtoto mchanga wakati wa kuzaliwa atachukuliwa hatua kwani inawezekana wapo baadhi yao ambao wanazembea na kushindwa kuwasaidia wajawazito pindi wanapofikishwa kwenye vituo kwa ajili ya kujifungua.
Alisema, mkakati mwingine ni watoa huduma za Afya kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili waweze kuvitumia vituo vya kutolea huduma za Afya, kwani itasaidia hata wilaya nyingine hapa nchini kuiga mfano wa Tunduru ambayo inakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo.
Renatus amewaonya watoa huduma kutojaribu kuzalisha mama wajawazito wenye mapacha kwenye zahanati na vituo vya Afya ambavyo hakuna huduma za dharura kwani wanaweza kusababisha madhara makubwa kwa mzazi na watoto.
“tunataka wilaya yetu iwe mfano bora kwa wilaya nyingine hapa nchini katika kumaliza tatizo la vifo vya mama na watoto wachanga na wale walio na umri chini ya miaka mitano”alisema, Renatus.
Pia Renatus ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kupitia Hospitali ya wilaya Tunduru ambayo imetenga vituo vitano vya dharura ambavyo Hospitali tatu na vituo vya Afya viwili.
Akifungua mafunzo hayo Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Wendy Robert alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuwavusha salama akina mama wote wajawazito wanaofika katika vituo kama mkakati wa wilaya ambao unataka kuona kuanzia mwaka 2020 hakuna mama mjazito anayepoteza maisha wakati wa kujifungua na wakato wote wa ujauzito wake.
Amewataka wahudumu wa Afya na watoa huduma za mama na mtoto kuhakikisha wanakuwa na lugha mzuri kwa wagonjwa na kujiepusha kutoa lugha chafu ambazo zinawakatisha tamaa wananchi wanaofika katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali kupata matibabu.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Maron Nyoni ameishukuru Ofisi wa Mganga Mkuu wa wilaya kwa kuwapatia mafunzo ambayo yanakwenda kuboresha suala la utoaji wa huduma Bora kwa wananchi.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa ni miundombinu hasa bara bara mbovu kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kumuwaisha mgonjwa pale anapohitaji huduma za dharura na kuiomba Serikali iendelea kuboresha bara bara zake hatua itakayosaidia sana kuokoa maisha ya wananchi hususani wagonjwa wanaohitaji rufaa.