*****************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewasihi wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanavaa Barakoa (Mask) kuanzia Jumatatu ya April 20 kila wanapokwenda kwenye maeneo ya Masoko na Vituo vya Daladala ili kujikinga na Janga la Virusi vya Corona.
RC Makonda pia ameelekeza wafanyabiashara wote wa mkoa huo kuhakikisha bidhaa wanazouza zinakaa kwenye vifungashio vya kubeba na kuondoka (Take away) ili kupunguza mikusanyiko.
Aidha RC Makonda ameyaomba Makampuni yote ya Simu za mkononi kuhakikisha miito ya simu (ring tone) zinatumika kutoa elimu ya kujikinga na Virusi vya Corona tofauti na ilivyo kwa sasa mtu akipiga simu anawekewa mziki.
Pamoja na hayo RC Makonda ameelekeza Viongozi wote wa masoko na Vituo vya daladala kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kumkinga kila mtu anaefika kwenye maeneo hayo huku akiendelea kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanazingatia umbali wa mita moja.
RC Makonda ametoa maelekezo hayo wakati alipokuwa akikabidhiwa Lita Laki moja sabini za kemikali inayotumika kutengeneza vitakasa mikono (sanitizer) kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya kwa lengo la kusaidia kupunguza kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ili kila mwananchi aweze kumudu kununua.