************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amekabidhiwa shehena ya Kemikali yenye ujazo wa Lita Laki moja na Sabini 170,000 kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwaajili ya Kutengeneza Vitakasa Mikono (Sanitizer) zitakazouzwa kwa punguzo la bei la 40% ili kumuwezesha kila mwananchi anaweza kumudu gharama na kujikinga na Corona.
RC Makonda amesema kemikali hizo zitatolewa kwenye viwanda vyote vinavyotengeneza Sanitizer vilivyosajiliwa na Serikali na vyenye utaratibu wa kuuza bidhaa zao kwa Bohari kuu ya Dawa MSD ambapo amesema atavielekeza Vyombo vya Ulinzi kupita na Kudhibiti kupanda kwa bei ya Sanitizer hizo.
Aidha RC Makonda ameelekeza kila Familia ikae kikao cha dharura ili wajiwekee mkakati na mbinu za kukabiliana na janga la Corona kuanzia ngazi ya familia huku akiwasisitiza wananchi kuendelea kuchukuwa tahadhari na kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya.
Kwa upande wake Kaimu Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya James Kaji amesema Kemikali hizo zilikamatwa na kutaifishwa na Serikali baada ya Kushinda kesi hivyo wameona ni vyema sasa kemikali hiyo ikatumika kupunguza mfumko wa bei ya Vitakasa Mikono (Sanitizer) ili kila mwananchi aweze kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.