Mkuu wa Takukuru Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
……………………………………………………………………………
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Manyara, inatarajia kufanya operesheni ya kuwakamata viongozi wa vyama vya ushirika waliofuja fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu aliyasema hayo akizungumza mjini Babati juu ya utekelezaji wa miezi mitatu ya Januari hadi Machi.
Makungu alisema kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo kipaumbele chao kitakuwa ufuatiliaji wa fedha za vyama hivyo vya ushirika na miradi mingine ya serikali.
“Tunafuatilia fedha za miradi ya vyama vya ushirika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli ya kufuatilia fedha za vyama vya ushirika zilizofujwa na baadhi ya viongozi wa ushirika,” alisema Makungu.
Alisema wameamua kutekeleza agizo la Rais Magufuli ili kubaini fedha za wakulima zilizofujwa na wajanja wachache kupitia vyama hivyo vya ushirika.
Alisema fedha ambazo zimesharejeshwa hadi hivi sasa ni asilimia 10 bado asilimia 90 zilizopo kwa wajanja wachache na wataendelea kuzifuatilia kwa ukaribu ili zirejeshwe.
“Tuna mipango endelevu ya kushirikisha umma katika mapambano dhidi ya rushwa katika maeneo mbalimbali ya Manyara kwenye vyama vyote vya ushirika,” alisema.
Alisema anampongeza Rais Magufuli kwa kutoa maagizo ya kufuatilia fedha za wanyonge zilizotafunwa na baadhi ya viongozi wa ushirika ili zirejeshwe.