Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Katavi
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu,Katavi
Matukio ya vitendo vya ubakaji kwa watoto wadogo wenye umri wa chini ya mwaka mmoja hadi miaka nane yameendelea kuripotiwa mkoani katavi ambapo idadi kubwa ya matukio hayo yanaelezwa kusababishwa na imani za kishirikina
Akizungumzia matukio hayo Afande Clara Ndamukyana wa kitengo cha Dawati la Jinsia mkoa wa Katavi amesema hali hiyo inasababishwa na waganga wa jadi wanaowadanganya wateja wao
“Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa wanasema waganga waliwaeleza kuwa wakipata mabinti ambao hawajaguswa katika tendo la ndoa ama watoto wadogo basi watafanikiwa kupata madini katika kazi zao za migodi au biashara nyingine” alisema Clara
Aidha ameeleza kuwa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita makosa mengi ya ubakaji yaliyoripotiwa yalikuwa ya wilaya ya Mpanda
Ameongeza kuwa sababu nyingine inayopelekea vitendo vya ubakaji ni watu kuamua tu kujistarehesha ambapo kundi hili kubwa linatokana na watu walio karibu na familia za waathirika wa ubakaji
Bi. Yustina Tizeba ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto mkoa wa Katavi; akizungumzia visa wanavyopokea katika Hospitali teule ya Rufaa ya mkoa amesema ndani ya wiki moja wanapokea kati ya mtoto mmoja hadi watoto tisa
Ameeleza kuwa wamekuwa wakipokea watoto wa kuanzia umri wa miezi kumi hadi miaka kumi na moja
Ameongeza kuwa hata watoto wa kiume wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili na kuingiliwa kinyume na maumbile
Dk. Tizeba ametoa ushauri kwa wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao hata mara moja kwa wiki na kuwaeleza namna ya kukwepa vitendo vya udhalilishaji ili kuwakinga watoto dhidi ya ubakaji
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa katavi wameilaumu serikali kwa kushindwa kuwaadhibu watuhumiwa wa vitendo hivyo na kuwaachia huru
Bakari Ndulumbi ni mkazi wa Makanyagio katika manispaa ya Mpanda anasema kuna mtu aliwahi kutambuliwa na wanafunzi wanne waliobakwa lakini polisi walimwachia huru
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amerudisha lawama kwa wananchi kwa kushindwa kutoa ushirikiano na hivyo kulazimu kuwaachia watuhumiwa bila kufikishwa mahakamani
“Unakuta unaita watu kutoa ushahidi wanaogopa aidha kwa kuwa ni ndugu wa ndani ndiye mbakaji” alisema Kamanda Kuzaga