********************************
April 17
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
KANISA la Christian Fellowship la Jijini Dar es Salaam limetoa viti mwendo Wheel Chairs 15 ,vyenye thamani ya zaidi ya milioni nne ,kwa ajili ya kituo kinachohudumia wagonjwa wa Covid 19 cha Lulanzi wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akikabidhi viti hivyo kwa mganga mkuu na mganga mkuu wa Halmashauri ya mji Kibaha na Dk Askofu Mgulu Kilimba wa kanisa hilo alisema lengo la kutoa viti hivyo ni kusaidia jitihada za serikali kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
“Nimetoa viti 15 kwa ajili ya kumuunga mkono Rais kwa ajili ya wagonjwa walioko pale ili watumie viti hivi wakati wa kupata matibabu yao kwani hii ni vita kubwa,” alisema Kilimba.
Aidha Kilimba alisema kuwa kwa sasa wameshatoa viti hivyo zaidi ya 4,000 nchini kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali na wabunge .
Nae mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Tulitweni Mwinuka alieleza, viti hivyo vitasaidia kutokana na kituo hicho kuwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya hospitali na vifaa tiba.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maji wa Kibaha alimshukuru Askofu Kilimba kwa msaada huo kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kwani hiyo ilikuwa moja ya changamoto za kituo hicho.
Kituo hicho ni moja ya vituo vya afya ambavyo vilipewa fedha na serikali kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambapo kwasasa serikali ilikifanya kuwa kituo cha kuhifadhi wagonjwa wa Corona baada ya tatizo hilo kutokea.