Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Edward Mapunda, akihubiri katika ibada ya Pasaka iliyofanyika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mkoani hapa.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Mchungaji Dkt. Alex Mkumbo (katikati) akiwa na baadhi ya wachungaji na waumini wa usharika wa Amani mkoani hapa, mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Pasaka
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa Anglican, Dayosisi ya Rift Valley mkoani hapa, Canon Joseph Kyense akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Pasaka
Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, Kanisa Kuu, Usharika wa Immanuel mkoani hapa, Mchungaji Dk. Syprian Hilinti akihubiri kwenye ibada ya pasaka ndani ya usharika huo hivi karibuni
Mchungaji Felix Kibiriti wa KKKT Dayosisi ya Kati, Usharika wa Immanuel Singida akizungumza kwenye ibada ya Pasaka iliyofanyika ndani ya usharika huo hivi karibuni
Waumini wa Kanisa Kuu Katoliki la Moyo Mtakatifu wa Yesu Singida wakishiriki ibada ya Pasaka.
Waumini wa KKKT Usharika wa Immanuel mjini Singida wakiwa kwenye ibada ya Pasaka.
Waumini wa KKKT Usharika wa Imanuel mjini Singida wakiwa kwenye ibada ya Pasaka.
Wanakwaya ya Msifuni ya KKKT Usharika wa Imanuel wakiimba nyimbo za Pasaka.
Kwaya ya Vijana ya KKKT Usharika wa Immanuel wakiimba.
Kwaya ya Vijana ya KKKT Usharika wa Imanuel wakiimba.
Wanakwaya ya Faraja ya KKKT Usharika wa Immanuel wakiimba wakati wa ibada ya Pasaka.
Wanakwaya wa Kanisa Kuu Katoliki la Moyo Mtakatifu wa Yesu wakiimba wakati wa ibada ya Pasaka
Na Godwin Myovela, Singida
VIONGOZI wa madhehebu tofauti ya kikristo mkoani hapa wamepongeza umakini na busara ya kipekee kwa Rais John Magufuli kwa maelekezo yake yanayozingatia uangalifu mkubwa kwa maslahi ya taifa ‘pasipo kukurupuka’ wakati huu ambapo watanzania wapo kwenye vita kali dhidi ya mlipuko wa janga la Corona.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Edward Mapunda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa ibada ya Pasaka alimpongeza Rais Magufuli kwa namna anavyolichukulia suala hili kwa umakini na uangalifu mkubwa kwa mtazamo mpana unaozingatia uhalisia wa maisha ya kila siku ya mtanzania.
“Lock down kwa watanzania wote sio nzuri, inaweza kuzalisha vifo na madhara mengine makubwa zaidi kutokana na msongo wa mawazo, njaa kwa hasa wale wanaotegemea kipato chao cha siku kujikimu,” anasema Mapunda na kuongeza:
“Kama watu wote watazuiwa kutoka nje basi kuna uwezekano wa vifo vingine visivyohusiana na ugonjwa wa corona kuongezeka zaidi kutokana na kukosekana kwa mabadilishano ya huduma …mathalani mgonjwa huyu wa TB anayehitaji maziwa kukosa wa kumletea na mengine mengi.”
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa Anglican, Dayosisi ya Rift Valley mkoani hapa, Canon Joseph Kyense, anasema anamshukuru Mungu kupitia Rais Magufuli kwa namna anavyolishughulikia suala la corona, huku akiwaomba watanzania kuzidisha maombi na kufuata maelekezo na tahadhari zinazoendelea kutolewa na mamlaka za nchi ili kwa pamoja tuweze kuvuka salama katika kipindi hiki kigumu.
Kyense anasema kauli ya Rais imejaa busara kutokana na ukweli kwamba kama tutafunga mipaka basi ni dhahiri huduma nyingine zitasimama, na kuna familia zinategemea kipato cha siku moja hivyo tukisema watu wasitoke ndani jamii itaathirika.
“Hali ya corona bado ni mbaya, na wagonjwa wanaendelea kuongezeka…kwenye ibada hii ya pasaka tulikuwa na maombi maalumu kuhusiana na ugonjwa huu tukielekeza maombi kwa Mwenyezi Mungu ili atuvushe salama katika kipindi hiki kigumu,” anasema Kyense na kuongeza:
“Nazingatia sana mawazo ya Rais, na ninampongeza kwa hekima yake katika hili, ninawasihi watanzania wenzangu tuendelee kuchapa kazi na kuchukua tahadhari zote kulingana na maelekezo yanayoendelea kutolewa na serikali…maambukizi bado yapo,” anasema.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, Kanisa Kuu, usharika wa Immanuel mkoani hapa, Mchungaji Dk. Syprian Hilinti kupitia mahubiri yake wakati wa ibada ya pasaka anawataka watanzania kuzidi kumtumainia Mungu dhidi ya janga hilo.
Hilinti anasema bila tumaini kwa Mwenyezi Mungu watu wataendelea kuteswa na ‘stess’ (msongo wa mawazo) na njaa kutokana na taharuki ya maradhi hayo, ikiwemo janga lililopo la mlipuko wa Virusi vya corona.
“Napongeza sana jitihada za serikali na hasa Rais Magufuli kwa jinsi anavyolikabidhi taifa hili kwa Mungu wakati wote anapoendelea kushughulikia suala la Corona, niwasihi wakristo wenzangu na taifa kwa ujumla tuzidi kumtumania Mungu tujikabidhi kwake… tusichoke kufanya maombi na tusikilize na kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya,” anasema Hilinti.
Hivi karibuni Rais Magufuli aliungana na Waumini wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kusali Ibada ya Ijumaa Kuu, na katika salamu zake alitumia fursa hiyo kutoa tathmini kadhaa ya hali halisi ya ugonjwa wa corona nchini na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali.
Anabainisha kuwa kutokana na madhara ya ugonjwa huo duniani, upo uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula, hivyo anawataka watanzania kuzalisha chakula cha kutosha na waendelee kuchapa kazi sambamba na kuhakikisha wanachukua tahadhari zote zinazostahili ili kujikinga ipasavyo na maambukizi ya Covid 19.
Aidha, anasisitiza kuwa kwa sasa serikali haitawazuia watu ndani ya nyumba zao, wala kufunga mipaka, kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kufanya hivyo.