Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma (hawapo pichani),wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari.
…………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna, Dodoma
Serikali imewahakikishia watanzania kuwa hakuna upungufu wa sukari Tanzania hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa ,wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari.
Mhe. Bashunga amesema kuwa kila mwaka serikali imekuwa makini katika kutathmini mahitaji ya sukari kwa wananchi na uwezo wa viwanda vya ndani katika uzalishaji.
Hata hivyo Mhe. Bashungwa amesema ni kweli bei ya sukari imepanda lakini haisababishwi na upungufu wa sukari bali imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na kirusi cha Corona.
“Ili kukabiliana na kadhia hiyo serikali imetoa vibali vya jumla ya Tani 40,000 kwa kampuni 4 za wazalishaji ambapo kila kampuni imeagiza Tani 10,000” ameeleza Mhe.Bashunga
Aidha Mhe. Bashungwa amesema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni Tani 9,990 na imeanza kutolea bandarini tangu jana jioni.
Pia Mhe. Bashunga amesema kuwa tarehe 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza jumla ya Tani 10,000 na Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza jumla Tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji huku Tani 1,800 ikiagizwa kutoka Afrika Kusini.
“wiki ya kwanza ya mwezi Mei Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza Tani 7,276 huku tarehe 15 Mei kampuni ya TPC itaingiza Tani 5,000 na Tarehe 30 Mei Tani 4,500 zitaingia nchini”, amebainisha Mhe.Bashunga.
Katika hatua nyingine Mhe. Bashungwa amesema kuwa Wizara inatarajia kuomba nyongeza ya Tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020
Hata hivyo amesema kuwa Asilimia 80% ya sukari ambapo kwa mujibu wa Takwimu mahitaji ya sukari inayotumiwa majumbani ni kiasi cha Tani 4,700,000 ambapo kati ya hizo Tani 378,000 zinazalishwa nchini.
Bashungwa amesema kuwa Hiyo ni hatua kubwa kwa nchi na serikali katika mkakati wa kuimarisha uchumi wa viwanda huku wawekezaji wengi wakiendelea na mchakato wa uongezaji tija na uwezo wa uzalishaji