Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma akizungumzia kuhusu matumizi ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia mtandao.
***************************
Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha- Mahakama
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Mawakili wamehimizwa kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupunguza msongamano wa watu mahakamani, kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona na kuokoa gharama za utoaji haki.
Akizungumza leo ofisini kwake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma alisema matumizi ya TEHAMA kwa watumishi na Mawakili yawe ni sehemu ya utendaji kazi wao wa kila siku ili kuendesha mashauri pasipokuwa na ulazima wa wananchi kufika mahakamani na hivyo kupunguza msongamano usio wa lazima.
‘‘Mashauri yote ya madai yanayohusisha mawakili yafunguliwe kwa njia ya mtandao na si vinginevyo,’’ alisema Msajili Mkuu.
Kanuni za ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (Electronic Filling Rules, 2018 GN 148/2018) iliyotolewa na Jaji Mkuu na kuanza kutumika Aprili 13, mwaka 2018 inasisitiza mashauri kufunguliwa kwa njia ya mtandao.
Alisema hivi sasa kuna Mawakili 1,732 waliojisajili katika mfumo wa kufungua mashauri kwa njia ya mtandao, lakini wanaoutumia ni 1,250. Hivyo alitoa wito kwa Mawakili hao, wakiwa kama Maofisa wa Mahakama kuona umuhimu wa kutumia mfumo huo hasa katika kipindi hiki cha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Kuhusu masuala ya utoaji wa elimu ya matumizi ya njia hiyo, Msajili Mkuu alisema Maafisa TEHAMA wa Mahakama kwa kushirikiana na Maafisa wengine wa Mahakama wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi wa kawaida juu ya mfumo huo.
Mhe. Chuma alisema viongozi wa kila ngazi ya Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani hadi Mahakama ya Wilaya wanapaswa kuhakikisha kuna kioski au sehemu maalumu yenye vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kusajili mashauri kimtandao ili kuwasaidia wananchi wasioweza kumudu kutumia huduma hiyo hususani wale wasio na uwakilishi.
Aliongeza kuwa Maafisa TEHAMA wahakikishe kwamba wanatoa msaada unaohitajika wakati wote katika maeneo hayo ili kufanikisha zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kuwapa haki wale wote wanaopaswa kupewa kwa mujibu wa taratibu.
‘‘Ni jukumu la kila Mtendaji wa Mahakama katika eneo lake kuhakikisha mahitaji muhimu yanapatikana ili kufanikisha zoezi hili, ’’alisisitiza.
Msajili Mkuu huyo aliwataka watendaji kushirikiana na maafisa TEHAMA katika maeneo yao kuhakikisha Majaji na Mahakimu wote wanatengenezewa sahihi za kielektroniki ndani ya siku 21 kupitia maagizo aliyoyatoa Aprili 14, mwaka huu.
Mhe. Chuma aliwataka viongozi wa Mahakama kudhibiti idadi ya waandishi wa habari wanaoingia maeneo ya Mahakama na kutoruhusu midahalo au mahojiano yoyote ya waandishi wa habari maeneo ya viwanja vya Mahakama kuanzia sasa ili kupunguza msongamano.
Kwa upande wa uendeshaji mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video Conference), alisema tayari taratibu za manunuzi zimeshafanyika ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo kwa Mahakama ambazo hazina. Alisema televisheni za ukutani 13 zitapelekwa katika magereza mbalimbali na saba (7) zitapelekwa kwenye vituo vya Mahakama Kuu. Aidha kompyuta mpakato 24 na scanner zitakazogawiwa kwenye maeneo hayo.
Machi 23, mwaka huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, katika Taarifa yake aliyoitoa kwa Umma aliwataka viongozi wote wa Mahakama katika ngazi zote kuonyesha uongozi kwa kuwasaidia Watanzania ili waendelee kupata huduma za utoaji haki katika dunia ambayo inapata msukosuko mkubwa wa ugonjwa wa Corona.