Mwenyekiti Mpya wa Chama cha Walimu (CWT ) Manispaa ya Singida, Hamis Mtundua, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT ) Manispaa ya Singida, Kitengo (KE), Yasinta Makiya, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT ndani ya Manispaa ya Singida wilayani hapa wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya viongozi wapya wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Singida wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuchaguliwa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika mkoani hapa leo. |
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Nchini (CWT ) Manispaa ya Singida, Hamis Mtundua (katikati), akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri kufungua mkutano.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri, akinawa mikono kabla ya kufungua mkutano wa uchaguzi wa CWT Manispaa ya Singida kama kinga ya kukabiliana na mlipuko wa Virusi vya Corona.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT ndani ya Manispaa ya Singida wakiwa kwenye mkutano huo.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT ndani ya Manispaa ya Singida wakiomba dua kabla ya kuanza uchaguzi kwenye mkutano huo.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT ndani ya Manispaa ya Singida wakipiga kura kuchagua viongozi.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT ) Mkoa wa Singida, Aran Jumbe, akizungumza kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti Mpya wa Chama cha Walimu (CWT ) Manispaa ya Singida, Hamis Mtundua na Msimamizi wa uchaguzi huo, Gabriel Gwaltu.
Na Godwin Myovela, Singida
CHAMA cha Walimu (CWT) Manispaa ya Singida kupitia mkutano wake mkuu wa kikatiba hatimaye kimefanikiwa kufanya uchaguzi kwa amani na kufanikiwa kupata viongozi wapya watakaohudumu ndani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Tofauti na mikutano mikuu na chaguzi za miaka ya nyuma, uchaguzi huo uliendeshwa kwa tahadhari kubwa chini ya ajenda moja pekee ya ‘uchaguzi’ ili kuhakikisha kila mjumbe anajikinga vilivyo na kufuata maelekezo stahiki dhidi ya mlipuko wa Virusi vya Corona.
Akizungumza jana mara baada ya kuchaguliwa kwa mara nyingine kuendelea kuongoza chama hicho, Mwenyekiti wa CWT Manispaa ya Singida mkoani hapa, Hamis Mtundua, alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake watajitahidi kupigania maslahi ya walimu wote hususani eneo la upandishaji wa madaraja.
Alisema kwa jitihada za chama hicho kwa kushirikiana na serikali, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita walifanikiwa kupandisha madaraja ya walimu takribani 500 ndani ya manispaa ya singida huku shabaha iliyopo mbele yao kwa sasa ni kufikisha idadi ya zoezi hilo kwa walimu stahiki 1200.
“Mpaka sasa upandishwaji wa vyeo umefanyika kwa walimu 539 na tunatarajia mda mfupi ujao zaidi ya walimu 1000 ndani ya manispaa yetu nao watapandishwa madaraja,” alisema Mtundua.
Aidha, akizungumzia sekta ya elimu kwa ujumla katika muktadha mzima janga la corona Mtundua alihamasisha serikali na jamii badala ya wanafunzi kukaa bure kusubiri ahueni ya mlipuko huo badala yake kujikita kwenye ufundishaji na utoaji elimu kwa njia ya mtandao.
“Katika hili jamii isibweteke, sasa ni wakati wa kujikita na suala la mtandao ili vijana wetu hawa ambao wapo majumbani wasikae bure bila kufundishwa na kujifunza sababu baadhi yao wanaweza hata kusahau walichofundishwa,” alisema.
Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri aliwataka viongozi wapya wa chama hicho kusimamia haki na maslahi ya walimu kwa mujibu wa malengo na katiba ya chama.
Aidha, Mulagiri katika kukabiliana na ugonjwa wa corona aliwataka walimu katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kusaidia jitihada zilizopo kwa kuelimisha jamii namna bora ya kujikinga na athari za mlipuko wa janga hilo kutokana na sekta hiyo kukubalika zaidi ndani ya jamii.
“Walimu tunawategemea sana katika nchi yetu, pia jamii inawakubali moja kwa moja. Kwa kipindi hiki ambacho tunapambana na corona tumieni nafasi hii wakati shule zimefungwa kulizungumzia hili,” alisema Mulagiri.