*******************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema agizo la kufungwa kwa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu litaendelea kubaki vile vile hadi hapo Serikali itakapotoa tamko jingine.
Pia, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesitisha maadhimisho ya Sherehe za Muungano (Aprili 26) pamoja na Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ili kuepuka msongamano na kuendelea kuzuia virusi vya corona visisambae zaidi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 14, 2020) katika kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Mapambano Dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu unaotokana na maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID-19). Amesema hadi leo, nchini kuna jumla ya watu 53 waliobainika kuwa na virusi vya corona ikiwa ni ongezeko la wagonjwa wanne ambao wote wapo jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali bado haijatangaza kuhusu kufunguliwa kwa shule, vyuo na shughuli za michezo pamoja na misongamano isiyokuwa ya lazima, hivyo maeneo hayo yataendelea kusalia katika karantini na wanafunzi wote wandelee kubakia majumbani kwao.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli ameagiza sh. milioni 500 ambazo zilitengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 56 ya Sherehe za Muungano zipelekwe kwenye mfuko wa kupambana na COVID-19 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia, Waziri Mkuu amewaomba wadau mbalimbali waendelee kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona kwani janga hilo ni kubwa na wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema elimu ya tahadhari ni muhimu ikaendelea kutolewa kwa wananchi ili waweze kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. “Kama si lazima kutoka, wananchi waendelee kutulia majumbani mwao.”
Amesema Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kusimamia utoaji wa elimu ya kujikinga na virusi hivyo hasa katika mkoa wa Dar es Salaam ambao unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi ikifuatiwa na Zanziba. “Ni muhimu wananchi wake wakapewa tahadhari juu ya namna ya kijikinga.”
Waziri Mkuu ameagiza kuwa wataalamu wanaosimamia utoaji wa huduma katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wa watu wenye maambukizi ya COVID-19, wakiwemo madaktari wote wapewe vifaa vya kijikinga ili kuhakikisha hawapati maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema watu waliokutana na wagonjwa waendelee kufuatiliwa kwa umakini na wahusika wawashirikishe viongozi wote hadi wa ngazi za chini na kwamba athari za kiuchumi zinazojitokeza kufuatia ugonjwa huo ziendelee kuchambuliwa.
Machi 17, 2020 na Machi 18, 2020, Serikali ilitangaza kuzifunga shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu kwa muda wa siku 30 na kwamba wanafuzi wa kidato cha sita waliopaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020 nao wangepaswa kusubiri Wizara ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.
Akitangaza uamuzi huo, Waziri Mkuu pia alisisitiza kuwa mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.
Alizitaka wizara na taasisi zizitishe semina, warsha, makongamano na mikutano yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki toka nchi zenye maambukizi makubwa. “Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” alisisitiza.
Akielezea hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ili kudhibiti ugonjwa huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyngine.