…………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeandaa mpango mkakati wa kukabiliana na msongamano wa magari ili kuleta adhi ya Jiji hilo.
Akizungumza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amesema kuwa watapiga marufuku malori ya mzigo kuanzia tani 10, kuingia katikati mji mara baada ujenzi wa barabara ya mzunguko kukamilika.
Oktoba 23, mwaka 2019, Serikali ilitangaza kujengwa kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 112.3 baada ya kupata fedha Sh.Bilioni 494 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ambapo ujenzi utafanyika kwa miezi 36.
Kunambi amebanisha mikakati hiyo kuwa ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kuondoa uharibifu na msongamano wa malori hayo katikati ya Jiji hilo.
“Magari makubwa ya mzigo kuanzia tani 10, hayataruhusiwa kuingia katika ya Mji,”amesema Kunambi.
Aidha Kunambi amesema kuwa jiji limeanza usanifu wa ujenzi wa reli kilometa 100 ndani ya Jiji hilo ili kujiepusha na tatizo la foleni ya magari.
Kunambi, ameongeza kuwa hivi sasa wameanza usanifu ujenzi huo ambao utalifanya Jiji hilo kutokuwa na foleni au msongamano wa magari.
“Treni hiyo itakuwa kiunganishi katika maeneo ya mji wa kiserikali Mtumba, uwanja wa ndege Msalato pamoja na maeneo yote ya barabara za mzunguko (Ring road),”amesema Kunambi
.
Hata hivyo Kunambi amesema kuwa miradi yote ya kimkakati katika jiji la Dodoma itakapokamilika itabadili kwa kiasi kikubwa muonekano na kuwa la kuvutia kuliko maeneo mengine nchini.