Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera akikata utepe kuzindua ofisi za wawekezaji hao
Moja ya trekta la kisasa zilizoletwa na kampuni ya Lonagro mkoani Katavi.
***********************************
Mkoa wa Katavi unaotegemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 80 umejipanga kufanya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji kutokana na uwekezaji katika zana za kisasa za kilimo
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa matrekta ya kisasa ya John Deer kutoka kampuni ya Lonagro inayojishughulisha na uuzaji wa matrekta mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera amevitaka vyama vya ushirika kuchangamkia fursa hiyo
“Kila AMCOS ichukue trekta;trekta litakusaidia kusomba mazao, kusomba matofali, na kazi nyingine kibao sio kulima tu” alisema Homera wakati akihutubia wakazi wa mkoa wa Katavi waliohudhuria hafla hiyo
Aidha baadhi ya viongozi wa wilaya akiwemo Mkuu wa wilaya ya Mlele Rachel Kasanda na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando wamesema ujio wa zana hizo za kilimo utafuta umaskini
Wameongeza kuwa kwa sasa mkoa una uwezo wa kuzalisha tani laki nne na nusu za mpunga na uzalishaji huo unategemea zaidi jembe la mkono lakini kwa kuwa zana za kisasa za kilimo wanaweza hata kufikia tani milioni tatu
“Kwa Maji Moto wanakuja wafanyabiashara kutoka Afrika ya Kusini kununua mchele tukizalisha zaidi mataifa mbalimbali yataongezeka na hivyo kukuza soko letu kwani tuna mchele mzuri sana” alisema Kasanda
Kwa upande wao baadhi ya wadau wa kilimo akiwemo mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara, kilimo, mifugo na viwanda Asanaly Dala wamewataka wakulima kutoyaangalia matrekta hayo kama picha na badala yake wayanunue na kuyatumia